JKT yakanusha ukatili kwenye mafunzo ya jeshi hilo
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) nchini Tanzania limewataka wananchi kupuuza taarifa za upotoshaji kupitia mitandao ya jamii na simu za mkononi kuhusu kuwepo kwa mateso na vitendo vya ukatili kwa vijana wanaojiunga na mafunzo yanayoendeshwa na jeshi hilo.
Akizungumza jijini Dar-es-Salaam Msemaji wa Jeshi la Kujenga Taifa Emmanuel Muruga amekanusha uvumi huo unaodai kuwa vijana wanaoendelea na mafunzo katika kambi za JKT kwa mujibu wa sheria huwa wanakufa kwa ukatili na kusema jambo hilo ni uzushi na upotoshaji.

