Mabondia Thomas Mashali [kulia] na Francis Miyeyusho wakiwa katika mazoezi ya pamoja.
Mabondia Thomas Mashali ambaye alifanikiwa kutwaa ubingwa wa dunia wa UBO uzito wa Super Middle baada ya kumshinda kwa pointi Sajad Mehrabi wa Iran usiku wa Jumamosi Uwanja wa Ndani wa Taifa, Dar es Salaam na mwenzake Francis Miyeyusho ‘Chichi Mawe’ ambaye naye alimshinda Ben Sajjabi wa Uganda kwa KO raundi ya pili pambano la uzito wa Super Bantam wamewataka wadau wa michezo nchini, makampuni, na Serikali kwa ujumla kuwekeza katika mchezo wa masumbwi.
Mabondia hao wametoa wito huo hii leo wakati wakizungumza na EATV michezo ilipotembelea maskani yao maeneo ya Kinondoni Stereo ambapo pia mabondia hao kwa pamoja waliwashukuru mashabiki wao kwakuwaunga mkono katika mapambano yao ya kulipwa yaliyofanyika mwishoni mwa juma lililopita katika uwanja wa ndani wa Taifa jijini Dar es Salaam na wote kuibuka na ushindi.
Miongoni mwa mambo ambayo walisisitiza mabondia hao ambao hufanya mazoezi yao kwa pamoja katika gym yao ya kazi kazi ni pamoja na uwekezaji katika vifaa vya mchezo huo ambavyo ni muhimu sana katika maandalizi na pia katika michezo yao ya ushindani.
Aidha pia wameitaka Serikali na wadau wenye uwezo hasa makampuni kuwekeza katika miundombinu ya kuchezea mchezo huo katika mazoezi na pia mashindano wakitolea mfano uwekezaji uliofanywa katika nchi mbalimbali kama Uingereza na Marekani nchi ambazo zina maeneo ama viwanja maalumu vya mchezo wa masumbwi ukizungumzia Mgm Grand Garden Arena na ule wa Manchester Arena ambavyo ni maarufu sana kwa michezo ya mapigano barani Ulaya na Marekani.
Wakimalizia wamesema iwapo Tanzania itafanikiwa kuwa na uwekezaji wa dhati utakaokidhi mahitaji ya mchezo wa masumbwi na sanaa zote za mapigano basi ni wazi mchezo huo utapiga hatua kubwa katika medani ya kimataifa na pia kikipatiakana kiwanja ama ukumbi maalumu wa mchezo huo wenye hadhi ya kimataifa kama ilivyo katika soka uwanja wa taifa ni wazi pia itakuwa rahisi kuleta heshima katika michezo wa ngumi na pia wageni maalumu kama viongozi wanaweza kufika kutazama michezo hiyo tofauti na mazingira ya sasa ngumi kufanyika katika kumbi za mabaa ama viwanja vya ndani vya michezo mingine kama mpira wa kikapu na kadhalika.