Mshambuliji Mbwana Samatta akiwajibika katika mchezo dhidi ya Sporting Charleroi.
Ndoto za mshambuliaji wa Kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta kucheza michuano ya Europa League mwakani zinaelekea kuwa ngumu kutimia baada ya jana usiku timu yake, ya KRC Genk kufungwa ugenini mabao 2-0 na Sporting Charleroi.
Katika mchezo huo wa kwanza wa mchujo wa mwisho kuwania nafasi ya mwisho ya kucheza Europa League uliofanyika Uwanja wa Pays de Charleroi mjini Charleroi, Samatta alianzia benchi kabla ya kuingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Yoni Buyens dakika ya 55.
Kufuatia kipigo hicho cha mabao ya Msenegali Amara Baby dakika ya 43 na Mfaransa Jeremy Perbet dakika ya 50, sasa Genk inatakiwa kushinda 3-0 katika mchezo wa marudiano Jumapili nyumbani ili kukata tiketi ya Ligi ya Uropa mwaka 2017.
Samatta jana amecheza mechi ya 17 tangu ajiunge na Genk akitoka kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na timu ya TP Mazembe pamoja na kutwaa tuzo ya Mwanasoka Bora anayecheza Afrika.
Katike mechi hizo, ambazo tisa ameanza, mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba SC ya Dar es Salaam, amefunga mabao manne, moja katika kila mechi Genk ikishindia 2-1 ugenini dhidi ya wenyeji SV Zulte-Waregem, 4-0 na 4-1 dhidi ya KV Oostende na 3-2 dhidi ya Club Brugge.
Kila la kheri kwa mshambuliaji huyo wa taifa Stars ambayo nayo kesho inashuka dimbani ugenini Jijini Nairobi Kenya kuvaana na wenyeji wao Harambee Stars katika mchezo wa kimataifa wa kalenda ya FIFA utakaotumiwa na timu zote mbili kujiwinda na michezo muhimu ya kuwania kufuzu kwa fainali za mataifa ya Afrika AFCON 2017, ambapo stars wao ambao kesho watamkosa Samatta katika mtanange huo watavaana na [Mafarao] Misri Juni 4 mwaka huu katika mchezo ambao Stars inahitaji ushindi wa si chini ya bao 4 kwa bila.
Na mara baada ya mchezo wao huko Ubelgiji mara moja Samatta maarufu kama Samagoals atarejea nchini tayari kwa mchezo dhidi ya Wamisri.