Jumatatu , 9th Mar , 2026

Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola ameijia juu ratiba ya soka nchini England, akidai mashindano ya vikombe vya ndani (EFL, FA) yanaonekana kupewa kipaumbele zaidi kuliko ratiba za michuano ya kimataifa (UEFACL, EUROPA)

Pep Guardiola

Guardiola ameonyesha kukerwa na ratiba inayoilazimisha timu yake kucheza dhidi ya Newcastle United katika hatua ya raundi ya tano ya FA Cup saa 2:00 usiku, Jumamosi, hali inayowapa muda mchache wa kupumzika kabla ya kusafiri kwenda kukutana na Real Madrid Jumatano katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.

"Hapa England, inaonekana kilichotokea kwenye EFL Cup ni muhimu zaidi kuliko mechi za kimataifa kwa timu za England. Hali hii imekuwepo tangu siku ya kwanza, hivyo si jambo la kushangaza.” Guardiola

Kocha huyo raia wa Hispania anaamini mamlaka zinazosimamia soka England hazisaidii vya kutosha klabu zao zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya kama ilivyo katika ligi nyingine Ulaya.

Guardiola alitolea mfano mchezo wa Real Madrid dhidi ya Celta Vigo ulihamishwa hadi Ijumaa ili kuwapa muda mzuri wa maandalizi, huku pia Paris Saint-Germain wakipangiwa ratiba ya ligi inayobadilishwa au hata kuahirishwa ili kurahisisha majukumu yao katika mashindano ya Ulaya.