Jumatano , 1st Jul , 2026

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetangaza kwa masikitiko kifo cha Suez Dani Maradufu, ambaye alikuwa dereva wa Makamu wa Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, John Heche.

Amani Golugwa (katikati) Naibu Katibu Mkuu CHADEMA Bara

Taarifa hiyo imetolewa baada ya marehemu kukutwa amefariki dunia leo Jumatano, Julai 1, 2026, katika chumba cha nyumba ya wageni aliyokuwa amefikia mjini Kigoma.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Amani Golugwa, mwili wa marehemu umechukuliwa na Jeshi la Polisi na kupelekwa Hospitali ya Mkoa wa Kigoma kwa ajili ya uchunguzi na taratibu nyingine zinazohusiana na tukio hilo.

Sababu ya kifo chake bado haijatangazwa rasmi huku uchunguzi ukiendelea.

Chama hicho kimetoa salamu za pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa, marafiki pamoja na wanachama wa CHADEMA walioathiriwa na msiba huo, kikisema kinaungana nao katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.