Ijumaa , 15th Apr , 2016

Ligi Kuu ya soka Tanzania bara VPL inatarajiwa kuendelea wikiendi hii kwa michezo minne kuchezwa katika viwanja mbalimbali nchini, huku kila timu ikisaka ushindi katika michezo hiyo ili kujiweka katika mazingira mazuri kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Kikosi cha mabingwa watetezi wa ligi kuu ya soka Tanzania bara VPL timu ya Yanga ya Dar es Salaam.

Kesho Jumamosi, kutakuwa na patashika kubwa baina ya mabingwa watetezi wa ligi hiyo Young Africans wao watakuwa wenyeji wa Mtibwa Sugar katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, huku Ndanda FC wakiwakaribisha wakata miwa wa Kagera Sugar katika uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.

Mchezo baina ya Yanga ambao ni wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya klabu bingwa Afrika na Mtibwa Sugar ni mchezo wa kisasi ikichukuliwa kuwa awali Yanga waliibuka na ushindi katika mchezo wa kwanza uliochezwa katika uwanja wa Jamhuri Mjini Morogoro lakini pia Mtibwa iliambulia kipigo katika michuano ya kombe la Mapinduzi hatua ya makundi.

Kutokana na hali hiyo kila upande umekiri waziwazi ugumu wa mchezo huo hasa kutokana na ubora wa vikosi vyao pia mazingira ya mchezo wenyewe.

Yanga wao wanataka ushindi ili kuwashusha kileleni vinara wa ligi hiyo Simba wenye alama 57 moja mbele yao huku Mtibwa wakitaka alama tatu ili kusaka nasasi ya tatu bora.

Mchezo mwingine utakuwa kati ya Wagosi wa Kaya Coastal Union watawakaribisha maafande wa JKT Ruvu katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga katika mchezo ambao Wagosi hao wa ndima watahitaji alama tatu kwa udi na uvumba ili kujinasua mkiani mwa ligi hiyo na kuanza kujinasua taratibu kwenye janga la kuporomoka daraja msimu ujao.

Jumapili, Simba SC wanacheza dhidi ya Toto Africans katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.