Jumanne , 19th Jul , 2016

Sasa idadi ya wanawake kushiriki Olimpiki kwa nchi ya Saudia, inaongezeka baada ya kamati ya Olimpiki ya nchi hiyo, kutangaza wanawake wanne kwenye timu ya Olimpiki, itakayokwenda Rio.

Sara Al-Attar atashiriki mashindano ya Olimpiki kwa mara ya pili baada ya kushiriki mashindano ya London 2012

Kamati ya Olimpiki ya Saudi Arabia imepitisha wachezaji wanawake wanne kujumuika kwenye timu ya Olimpiki ya nchi hiyo inayojiandaa na mashindano ya Olimpiki ya Rio.

Kamati ya Olimpiki ya Saudia, imeeleza kuwa, Sara Al-Attar, Lubna Al-Omair, Cariman Abu Al-Jadail na Wujud Fahmi, watapewa nafasi za upendeleo (wildcard entries) bila ya mashindano ya mchujo.

Saudi Arabia ilijumuisha kwa mara ya kwanza wanawake wawili kwenye fainali za Olimpiki za mwaka 2012, jijini London, baada ya kamati ya Olimpiki, kuruhusu uvaaji wa hijab na suruali kwa wanamichezo wa kike wa nchi zinazofata imani ya dini ya kiislamu.