Bondia Thomas [Mashali kushoto] akijifua na mkongwe Rashid Matumla.
Mabondia Thomas Mashali wa Tanzania na mpinzani wake Sajjad Mehrab wa Iran hapo jana wamepima uzito na afya zao tayari kabisa kwa mpambano wa kimataifa wa raundi 12, kuwania ubingwa wa dunia wa UBO uzito wa juu mwepesi mpambano utakaofanyika jijini Dar es Salaam leo.
Katibu mkuu wa shirikisho la ngumi za kulipwa Tanzania PST ambao ndiyo wasimamizi wa ndani Anthon Ruta amesema maandalizi ya mpambano huo na mengine ya utangulizi yamekamilika huku bondia Thomas Mashali ambaye alikuwa akinolewa na Mkongwe Rashid Matumla yeye akiahidi kuibeba Tanzania leo..
Aidha Ruta amesema mabondia wote wawili wametimiza vigezo vyote vya mchezo wao ambapo Thomas Mashali 'Simba Asiyefugika' atakuwa anagombea ubingwa wa dunia kg 76 mkanda wa U.B.O na Sajjad Mehrab kutoka 'Irani' baada ya wote kulingana uzito na kuwa na afya njema.
Pamoja na mpambano huo mkubwa pia hiyo kesho kutakuwa na patashika nyingine kwa mapambano mengine ya kimataifa yatakayowakutanisha mabondia Mwanadada Lulu Kayage atakaezichapa na Chiedza Homakoma 'Nikita' wa Malawi na Allen Kamote atapambana na Salim Chazama wa Malawi.
Mapambano mengine ni kati ya Ramadhan Shauri atakayepambana na Osgood Kayuni wa Malawi wakati Twaha Kassim atapambana na Fred Nyakese kutoka Kenya na Saleh Mkalekwa atakumbana na Jems Onyango wa Kenya
Na mbishi kutoka Kinondoni Fransic Miyeyusho 'chichi mawe yeye atavaana na Sajjabi Ben wa Uganda na Nassibu Ramadhani atacheza na Edwrd Kakembo wa Uganda hayo yakiwa ni mapigano ya kimataifa huku mapambano mengine ya kitaifa yatawakutanisha Shaban Kaoneka atakaecheza na Hassan Mwakinyo na Issa Nampepeche atakumbana na Baina Mazola pambano ambalo kocha wa Kimataifa wa mchezo wa masumbwi nchini Rajabu Mhamila 'Super D' ameahidi kutoa zawadi binafsi ya vifaa vya mchezo wa ngumi kwa mshindi kati ya Nampepeche na Mazola.
Akimalizia Ruta amesema siku hiyo pia kutakuwa na ugawaji wa zawadi kwa mabondia watakaocheza vizuri na kuonesha nidhamu ya mchezo wa masumbwi watapata zawadi mbalimbali ikiwemo vifaa vya mchezo pamoja na DVD za mafunzo ya mchezo wa ngumi pamoja na kutambua shiria za mchezo huo.