Jumatano , 8th Jul , 2015

Kikosi cha wachezaji wa Timu ya Azam FC kinatarajiwa kuondoka kesho kuelekea jijini Tanga ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na kati ngazi ya Klabu kama Kombe la Kagame.

Akizungumza na East Africa Radio, Afisa habari wa Azam FC, Jaffary Iddy Maganga amesema, kikosi hicho kinatarajia kuwa na mechi mbili jijini humo ambapo mechi ya kwanza inatarajiwa kuchezwa Julai 11 dhidi ya African Sports na Julai 12 watashuka kucheza dhidi ya Coastal Union.

Maganga amesema, mashindano ya Kagame ni kipimo kwa kocha kuangalia kitu gani kinaendelea kwenye timu na kujua mapungufu yaliyopo katika timu na kuweza kuongeza na kujua wachezaji wamepokea vipi mazoezi anayoyatoa.

Maganga amesema, mpaka sasa wamecheza mechi mbili za kirafiki ambapo hapo awali walicheza na Friends Rangers ambapo walishinda bao 4-2 na hapo jana walishuka kucheza na JKT Ruvu ambapo walishinda bao 1-0.

Maganga amesema, wachezaji waliokuwa wakiitumikia timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars bado hawajaanza mazoezi na bado wataendelea kuwa katika mapumziko ya muda mfupi kwa ajili ya kujiweka sawa ili kujiandaa na michuano ya Ligi kuu Soka Tanzania Bara.