Alhamisi , 17th Feb , 2022

Kiungo bora wa Ligi kuu soka Tanzania bara msimu uliopita Clatous Chama amezidi kuonyesha ubora wake katika soka la Tanzania baada ya hapo jana kufunga mabao matatu Hat-trick kwenye mchezo wa Azam Sports Federation Cup na kumfanya awe amehusika kwenye mabao 8 katika michezo 6.

Clatous Chama amehusika kwenye mabao 8 katika michezo 6

Msimu uliopita Chama alikuwa ndio mchezaji aliyehusika kwenye mabao mengi kwenye ligi kuu soka Tanzania bara baada ya kufunga mabao 8 na kutoa pasi za magoli (Asisst) 15 na kumfanya kuhusika kwenye mabao 23 ambayo ilikuwa ni idadi kubwa kuliko mchezaji yeyote yule, ubora huo ulimfanya ashinde tuzo ya kiungio bora wa msimu. Lakini pia kiwango hicho kiliwavutia klabu ya RS Berkane ya Morocco kumsajili .

Lakini mambo hayakumuendea vizuri akiwa na Berkane ambapo ilitajwa changamoto za nje ya uwanja zilimfanya kiungo huyo mshambuliaji raia wa Zambia kuvunja mkataba na klabu hiyo na kurejea tena Tanzania katika klabu ya Simba SC  kwenye dirisha dogo la usajili lilofungwa Januari 15 mwaka huu 2022.

Toka aliporejea tena katika klabu ya Simba mwamba wa Lusaka tayari ameshacheza michezo 6 kwa ujumla kwenye michezo ya Ligi kuu na ya Azam Sports Fedaration Cup na katika michezo hiyo Chama amehusika kwenye mabao 8 akiwa amefunga mabao 5 na amatoa pasi za usaidi wa magoli (Asisst) 3.

Wachezaji wa Simba wakipongeza baada ya ushindi wa bao 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting

Amefikisha idadi hiyo baada ya hapo jana kufunga mabao 3 kwenye mchezo wa dhidi ya Ruvu Shooting ambao Simba iliibuka na ushindi wa mabao 7-0 lakini pia alitoa pasi moja ya goli, Chama pia alifunga bao 1 kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mbeya Kwanza ambao Simba ilishinda kwa bao 1-0, na kwenye mchezo wa raundi ya 4 wa ASFC dhidi ya Dar City alifunga bao 1 na alitoa pasi 2 za mabao.

Kiungo huyo anaweza kutanua wigo huo wa takwimu kwani bado kuna michezo 15 ya Ligi Kuu soka Tanzania bara kabla ya msimu kumalizika, lakini pia Simba imefuzu hatua ya robo fainali ya michuano ya Azam Sports Federation Cup.