Jumapili , 5th Jan , 2025

Jaji katika mahakama ya New York Juan Merchan anayesikiliza kesi ya utoaji hongo dhidi ya rais mteule wa Marekani Donald Trump anatarajiwa kutoa uamuzi juu ya kesi hiyo siku 10 kabla ya kuapishwa kwake Januari 20.

Donald Trump, Rais mteule wa Marekani

Jaji Merchan amesema Trump, Rais wa kwanza wa zamani kuwahi kuhukumiwa kwa uhalifu, anaweza kujitokeza ana kwa ana au kwa njia ya mtandao katika hukumu iliyopangwa kusomwa Januari 10.
Katika uamuzi wa kurasa 18, Merchan alikataa hoja mbalimbali za mawakili wa Trump wakitaka hukumu yake kutupiliwa mbali.

Jaji huyo amebainisha kwamba hana nia ya kutoa adhabu ya kifungo jela, badala yake anaegemea katika kuachiliwa bila masharti, hukumu nyepesi ambayo hata hivyo itamfanya Trump aingie Ikulu ya White House kama mhalifu aliyepatikana na hatia. Trump anatarajiwa kukata rufaa ambayo inaweza kuchelewesha hukumu yake.

Trump alipatikana na hatia huko New Yorkmnamo mwezi Mei kwa makosa 34 ya kughushi rekodi za biashara ili kuficha malipo ya pesa kwa nyota wa filamu za ngono Stormy Daniels kabla ya uchaguzi wa 2016.

Mawakili wake walikuwa wakitaka kesi hiyo itupiliwe mbali kwa misingi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na uamuzi wa kihistoria wa Mahakama ya Juu mwaka jana kwamba marais wa zamani wa Marekani wana kinga ya kutoshtakiwa kutokana na vitendo mbalimbali vya kiofisi vilivyofanywa wakiwa madarakani.Trump apatikana na hatia katika kesi ya uhalifu

Hata hivyo Jaji Merchan alikataa hoja hiyo lakini alibainisha kuwa Trump hataweza kushtakiwa mara tu atakapoapishwa kama rais.

Msemaji wa Trump, Steven Cheung ameshutumu uamuzi wa Jaji Merchan wa kutoa hukumu kwa rais huyo wa zamani, akiuita "ukiukaji wa moja kwa moja wa uamuzi wa kinga ya Mahakama ya Juu na sheria zingine za muda mrefu."Kesi ya kihistoria dhidi ya Trump yaanza New York

"Kesi hii ya uvunjaji sheria haikupaswa kamwe kuletwa na Katiba inataka itupiliwe mbali mara moja," alisema Cheung katika taarifa yake.