Mtoto mwenye kansa ya macho apata msaada

Jumanne , 16th Feb , 2021

Kampuni ya michezo ya kubashiri nchini ya Meridian Bet, imemsaidia kiasi cha shilingi millioni Moja kwa mtoto Rehema Faustine (1), aliyezaliwa na kansa ya macho hali iliyopelekea kushindwa kuona wala kusikia huku baba yake akimtelekeza mtoto huyo kutokana na hali yake.

Meridian Bet wakikabidhi kiasi cha shilingi milioni moja kwa Nadia Faustine, mama wa mtoto mwenye kansa ya macho

Awali akisimulia, mama mzazi wa mtoto huyo Nadia Faustine (24), amesema kuwa amebahatika kupata mtoto mmoja aitwaye Rehema ambaye amezaliwa na ulemavu wa macho baada ya kupata kansa ya macho akiwa tumboni.

Akisimulia kwa uchungu Nadia amesema alipata ujauzito na baada ya miezi 4 akaambiwa ana watoto mapacha tumboni lakini mmoja amefariki mmoja mzima hivyo akaambiwa asubirie hadi miezi sita ili yule mzima akue hali iliyopelekea matatizo makubwa kwa mtoto aliyekuwa hai.

Akizungumza wakati akitoa msaada huo, Meneja Ustawi wa Meridian Bet Amani Maeda, amesema wameguswa na matatizo anayoyapitia mtoto huyo hivyo wakaguswa kumsaidia ili aweze kupata matibabu zaidi

Naye Mkuu wa Utawala kutoka Meridian Bet, Cornelius Bornman, amesema kampuni hiyo imekuwa ikishiriki katika matukio mbalimbali ya kijamii kwa lengo la kusaidia jamii zenye uhitaji huku akionesha kusikitishwa na matatizo ya mtoto huyo.

Kwa upande wake Nadia Faustine, ameishukuru kampuni ya Meridian Bet kwa kumsaidia mtoto wake fedha kwa ajili ya matibabu kwani anapitia katika wakati mgumu kutokana na matatizo aliyonayo.

Kwa sasa mtoto huyo anatakiwa kufanyiwa upasuaji ili kutolewa mabaki ya macho yaliyosalia ili yasimsababishie matatizo kwenye mishipa ya fahamu ambapo gharama yake ni kiasi cha shilingi milioni moja na laki tano.