Alhamisi , 23rd Feb , 2017

Watu saba (07) wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa kosa la kupatikana wakiwa na dawa za kulevya zinazodhaniwa kuwa ya heroine kiasi cha kete 32, bhangi kilo mbili na nusu na misokoto 75 ya bangi, wilayani Nyamagana, Mkoani Mwanza.

DCP Ahmed Msangi - RPC Mwanza

Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza Naibu Kamishina wa Polisi Ahmed Msangi amesema tukio hilo limetokea tarehe 22.02.2017 majira ya saa 4 asubuhi katika maeneo ya katikati mwa jiji la Mwanza.

Kamanda Msangi amesema kuwa polisi bado wapo katika mahojiano na watuhumiwa wote saba, ili kuweza kubaini mtandao wa watu wanaoshirikiana katika biashara hiyo haramu ya dawa za kulevya na kuwa uchunguzi ukikamilika watuhumiwa wote saba watafikishwa mahakamani kwa ajili ya hatua stahiki za kisheria.

Aidha Kamanda Msangi amesema kuwa oparesheni ya dawa ya kulevya ni endelevu katika maeneo yote ya jiji na mkoa Mwanza na kuwataka wananchi waendelee kutoa taarifa mapema polisi kuhusu watumiaji, wauzaji na wasafirishaji wa dawa hizo, ili waweze kukamatwa kisha wafikishwe katika vyombo vya sheria.