Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara linamshikilia Mhandisi Wilson Charles, Meneja wa TARURA mkoa wa Kagera kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya Rhoda Jonathan (46), mkazi wa Kitongoji cha Burunga, Kata ya Uwanja wa Ndege, Wilaya ya Serengeti mkoani Mara.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo, amethibitisha kushikiliwa kwa mume wa marehemu kwa uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo, ambapo Rhoda Jonathan aliuawa kikatili kwa kukatwa mapanga hadi kufa.
Tukio hilo lilitokea usiku wa Oktoba 23, 2025, majira ya saa moja na nusu usiku, nyumbani kwa marehemu, ambapo inadaiwa watu wawili waliruka ukuta na kuingia ndani kabla ya kutekeleza mauaji hayo.
Marehemu alikuwa mke wa Mhandisi Wilson na wawili hao wamejaliwa watoto watatu. Imeelezwa Marehemu na mtuhumiwa hawakuwa wakiishi pamoja kwa takriban miaka mitano, lakini walikuwa wakiwasiliana.
Mashuhuda walisema mwili wa marehemu ulikutwa umekatwa mapanga sehemu mbalimbali, ikiwemo kiganja cha mkono wa kulia kilichokatwa na kuachwa chini, huku mwili wake ukiwa pembeni ya kitanda na majeraha makubwa kifuani, mdomoni na mikononi.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Burunga, James Makuru Marwa, alithibitisha tukio hilo na kueleza kuwa alipokea taarifa kutoka kwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Serengeti kabla ya kufika eneo la tukio na kuongeza kuwa, siku iliyofuata, panga lenye damu lilipatikana jirani na eneo la tukio, na Polisi walilikusanya kwa ajili ya uchunguzi zaidi
Aidha, Kijana aliyekuwa akiishi nyumbani kwa marehemu, Mophati Mwita (14), alieleza kuwa wakati alipokuwa jikoni akipika, mwanafunzi aliyepanga nyumbani hapo alimwona mtu akiruka ukuta na kuingia ndani.
Pia, kufuatia msiba huo umebuka mzozo mkubwa kati ya familia za marehemu na mtuhumiwa, huku kila familia inataka msiba uwekwe kwao.

