
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amempa siku tano (5) Mohamed Mstafa kujisalimisha kwenye ofisi ya Mkuu wa mkoa kabla ya hatua zaidi hazijachukuliwa kuhusiana na sakata la nyumba lililomhusisha na mjane Bi. Alice Haule.
RC Chalamila ametoa kauli hiyo leo Oktoba 20 jijini Dar es Salaam mara baada ya ya kukabidhiwa hati miliki ya kiwanja ilipo nyumba hiyo ambayo ameikabidhi kwa mjane Bi. Haule pamoja na kiasi cha shilingi 10 kwa ajili ya kuanzia maisha.
Aidha, RC Chalamila amebainisha kuwa Bwana Mstafa amekuwa na maelezo yasiyoeleweka katika maelezo yake huku akiviagiza vyombo vya Dola kuendelea kutafata Mohamed kwa kutumia majina ya viongozi katika maelezo yake kwa kujinasibu kuwa amekuwa na urafiki wa karibu na viongozi.
Kwa upande wake Kamishina msaidizi wa ardhi mkoa wa Dar es Salaam Shukrani Kiyando amesema baada ya kupokea maoni kutoka kwenye timu iliyoundwa kufanya uchunguzi wameamua kuwa haki ya umiliki wa nyumba urudishwe kwa Bi. Alice Haule.
Akizungumza mara baada ya kupokea hati hiyo,Bi. Alice Haule amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wanyonge na Pamoja na Mkuu wa Mkoa na vyombo vya habari kwa kushirikiana katika kupata haki yake.