Jumapili , 26th Oct , 2025

"CWT pia inawahakikishia waalimu, serikali na wananchi wote kuwa tutaendelea kushirikiana na mamlaka husika kuhakikisha kuwa tabia hii ya utoaji taarifa potofu inakomeshwa ili kulinda misingi na madhumuni ya uwepo wa vyama vya wafanyakazi kwa mujibu wa sheria."

Chama cha waalimu Tanzania (CWT) kimekanusha vikali taarifa zinazosambazwa kwenye baadhi ya Mitandao nchini na baadhi ya Vyombo vya habari zikihamasisha waalimu kutoshiriki kwenye uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 kwa maelekezo kuwa ni msimamo wa Chama hicho Taifa.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa CWT Mwalimu Joseph Misalaba leo Jumapili Oktoba 26, 2025 kwenda kwa Makatibu wa Mikoa imetoa rai pia kwa waalimu na wanachama wa CWT kupuuza taarifa hizo kwani hazina ukweli wowote na zinalenga kuzua taharuki, uzushi na uchonganishi ambao unapaswa kupingwa ili kuendelea kulinda umoja, amani na utulivu ambao ni tunu ya Tanzania.

"CWT pia inawahakikishia waalimu, serikali na wananchi wote kuwa tutaendelea kushirikiana na mamlaka husika kuhakikisha kuwa tabia hii ya utoaji taarifa potofu inakomeshwa ili kulinda misingi na madhumuni ya uwepo wa vyama vya wafanyakazi kwa mujibu wa sheria." Amesema Mwalimu Misalaba katika taarifa yake kwa umma.

CWT pia imewataka waalimu wote nchini kuendelea na msimamo wao wa kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025 kwenda kupiga kura kwani ndiyo msimamo wa Chama hicho ambao ulishatolewa na Msemaji wa CWT ambaye ni Rais wa Chama hicho.

Kimewasisitiza pia Waalimu na umma wa Watanzania kuwa mabalozi wazuri wa upendo, amani, umoja na mshikamano kwaajili ya maendeleo thabiti ya Taifa la Tanzania, wakiishukuru pia serikali kwa kuendelea kutatua kero mbalimbali za Waalimu kwa kushirikiana na Chama cha Waalimu Tanzania (CWT).