Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo
Mvua hiyo ambayo imetajwa kuwa kubwa kuliko zote tangu msimu wa mvua kwa mwaka huu uanze jijini humo, ilidumu kwa takribani masaa matano na kusababisha mafuriko makubwa yaliyopelekea uharibifu mkubwa wa miundombinu ya barabara na makazi ya watu, ikiwemo vitu vya ndani.
Kufuatia hali hiyo, www.eatv.tv ililazimika kufuatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Arusha kutembelea maeneo ambayo yameathirika zaidi na kuchukua hatua za dharula za uokoaji huku Mkuu wa Mkoa, Mrisho Gambo, akiwataka Wakurungenzi wa Halmashauri za jiji kutowachukulia hatua watumishi wote waliochelewa kazini kwa siku ya leo.
"Baada ya kupita mimi pamoja na viongozi wenzangu kujionea hali halisi, natoa maelekezo kwa wataalam wote, wataalam wa ardhi na TARURA na TANROADS, wapite kwenye maeneo haya waangalie athari zilizopo na baada ya hapo watuletee tathmini, mapendekezo na hatua za kuchukua", amesema Mrisho Gambo.
Maeneo makubwa yaliyoathirika na mvua hizo ni yale yaliyo na ujenzi holela wa makazi na usiofuata kanuni.
Hata hivyo hakuna mathara ya kifo au majeruhi iliyoripotiwa kutokana na mvua pamoja na mafuriko hayo.
Tazama hapa chini viongozi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wakizungumza.