Mafuta ya kula
Hayo yameelezwa bungeni leo Aprili 22, 2021 na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe wakati akijibu swali la mbunge wa Viti Maalum Mhe. Mariam Ditopile Mzuzuri lililohoji, Serikali ina mkakati gani wa kuwawezesha wakulima nchini kuwekeza katika kilimo cha mazao ya Alizeti, Michikichi na Karanga ili kuokoa kiasi cha fedha zinazotumika kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi.
Mhe. Bashe amebainisha kuwa nchi hutumia wastani wa shilingi bilioni 474 kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi kwa mwaka.
Aidha, ameeleza kuwa katika kuhakikisha uzalishaji wa mbegu za alizeti unaongezeka katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imeiwezesha ASA jumla ya shilingi bilioni 3 kwa ajili ya kuzalisha mbegu za alizeti. Vilevile, kwa mwaka wa fedha 2021/2022. Pia Serikali imepanga kuiwezesha ASA shilingi bilioni 10.6 ili kuzalisha tani 5,000 za mbegu ya alizeti kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa mbegu za mafuta.
Amefafanua kuwa serikali imeona umuhimu wa kuwekeza kwenye mazao ya kuzalisha mafuta ambapo uwekezaji huo unatekelezwa chini ya mikakati ya kutatua changamoto katika sekta ya uzalishaji mafuta kwa kushirikisha Wizara ya Kilimo, Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Viwanda na Biashara. Mikakati hiyo imelenga kutatua changamoto ya uzalishaji wa mbegu za mafuta ili kujitosheleza kwa mahitaji ya ndani ya nchi.