Ndege ya ATCL
Kwa mujibu wa msemaji mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbas, amesema baada ya kusikilizwa kwa shauri la kesi hiyo leo mahakamani hapo, huku jopo la majaji kutoka Tanzania wakiwepo, mahakama imeamua kuachiwa kwa ndege.
''Mahakama Kuu ya Gauteng, Afrika Kusini, leo imetoa hukumu na kuamuru kuwa ndege ya Air Tanzania, iliyokuwa ikishikiliwa nchini humo iachiwe na mlalamikaji alipe gharama za kesi'', amesema Msemaji.
Aidha Dkt. Hassan Abbas amewashukuru Watanzania kwa kuwa wavumilivu ambapo amesema, ''tunawashukuru wote kwa uvumilivu wenu''.
Mapema jana Waziri wa Uchukuzi Mhandisi Isack Kamwelwe aliwaasa watanzania kuendelea kuwa wavumilivu juu ya ndege hiyo, kwasababu juhudi kubwa zilikuwa zinafanyika ili kuiokoa.
Ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) ilishikiliwa nchini Afrika ya Kusini Agosti 24,2019, kwa amri ya Mahakama nchini humo, kutokana na kesi iliyofunguliwa na raia mmoja wa huko.