Ahmed Msangi
Taarifa ya jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza imeeleza kwamba tarehe 30.07.2016 majira ya saa 4:30 asubuhi katika kitongoji cha Bukini kijiji cha Chifule kata ya Bukungu tarafa ya Ukara wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Zephania Bita miaka 42 mfanyabiashara na mkazi wa kitongoji cha Bukumia alifariki dunia kwa ajali ya moto uliowaka wakati wakimimina mafuta aina ya petrol na mwenzake aliyejulikana kwa jina moja la Dotto ambaye amejeruhiwa katika sehemu mbalimbali za mwili wake.
Inadaiwa kuwa marehemu alikuwa ndani ya nyumba yake chumbani na mwenzake tajwa hapo juu, hivyo wakati wanamimina mafuta hayo ya petrol kwenye madumu alipita mtu kwenye korido ya nyumba hiyo akiwa anavuta sigara na kupelekea kuzuka kwa moto uliomuunguza marehemu mwili mzima na kusababisha majeraha bwana Dotto ambaye hali yake bado sio nzuri.
Aidha moto huo umesababisha madhara mengine ya kuungua kwa vyumba vinne pamoja na kuteketea kwa mali zilizokuwepo ndani ya nyumba hiyo, thamani halisi ya vitu na mali zilizoteketea katika ajili hiyo bado haijafahamika,.
Taarifa hiyo imesema kuwa majeruhi amelazwa hospitali ya wilaya ya Ukerewe kwa matibabu na kwamba hali yake bado sio nzuri.
Jeshi la polisi bado linaendelea na uchunguzi kuhusiana na ajali hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Naibu Kamishna wa Polisi Ahmed Msangi ametoa wito kwa wakazi wa jiji na mkoa wa Mwanza akiwataka kujihadhari wakati wote pindi wanapofanya kazi za hatari ili kuweza kuzuia ajali na vifo vinavyoweza kuepukika, lakini pia amewataka watu wenye tabia ya kufanya biashara za mafuta ya petrol na diesel zisizo halali kisheria kuacha mara moja.








