Jumamosi , 3rd Jan , 2015

Idadi kubwa ya abiria wanaosafiri kutoka mkoani kilimanjaro kuelekea mikoa mingine hapa nchini wamekwama katika kituo kikuu cha mabasi cha mjini Moshi.

Idadi kubwa ya abiria wanaosafiri kutoka mkoani kilimanjaro kuelekea mikoa mingine hapa nchini wamekwama katika kituo kikuu cha mabasi cha mjini Moshi baada ya kukosa usafiri wa mabasi makubwa kutokana na ongezeko kubwa la abiria waliokuja kusherehekea sikukuu za krismas na mwaka mpya.

Wakizungumza katika kituo kikuu cha mabasi mjini moshi baadhi ya abiria wamesema kuwa wameshindwa kuendelea na safari kutoka na kukosa tiketi kufuatia wingi wa abiria wanaosafiri na hivyo kusababisha mabasi hayo kujaa abiria.

Kufuatia adha hiyo abiria hao wameiomba mamlaka ya usafiri wa nchi kavu na majini SUMATRA kuruhusu magari madogo aina ya COASTER kusafirisha abiria ili kupunguza msongamano wa abiria katika kituo hicho.

Kwa upande wake kiongozi wa usafirishaji katika kituo cha mabasi mjini Moshi Bw. Daniel Kimwaga amesema mabasi madogo hayana kibali cha biashara cha kusafirisha abiria kwenda mikoani vinginevyo mamlaka ya usafiri wa nchi kavu na majini SUMATRA iangalie uwezekano wa kuruhusu magari ambayo yana uwezo wa kusafirisha abiria ili kukabiliana na tatizo hilo.