Alhamisi , 26th Mei , 2022

Tume ya ushindani FCC kwa kushirikiana na Tume ya ushindani halali ya Zanzibar ZFCC zimejipanga kudhibiti uingizaji na uzalishaji wa bidhaa bandia ili kuchochea uchumi utakaolinda soko la ndani na Kumlinda mlaji 

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani Tanzania (FCC) William Erio amesema hayo wakati wa kuhutimisha ziara ya kikazi ya siku tatu kwaajili ya kutembelea  Tume ya Ushindani Tanzania (FCC) ikiwa na lengo la kuimarisha mahusiano na kuangalia namna bora ya kutekeleza majukumu yao.

"Suala la biashara  si suala la muungano, kwahiyo sisi FCC tunashughulika na masuala haya ya kibiashara kwa maana ya kushajihisha ushindani, kulinda washindani katika shughuli zao na kumlinda mlaji kwa Tanzania bara ambapo na wenzentu wanafanya hivyohivyo kwa upande wa Tanzania Zanzibar" Alisema William Erio ambaye ni Mkrugenzi Mkuu Tume ya ushindani Tanzania FCC

Aidha Mkurugenzi huyo alisema Serikali ya awamu ya sita imejikita katika kuimarisha uwekezaji Kama njia mojawapo Kuu ya kuleta mitaji na kukuza uchumi wa nchi yetu Kama vile inavyofanya serikali ya awamu ya nane kule Tanzania Zanzibar.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani halali ya biashara Mohammed Sijari Mohammed amesema  kuwa Zanzibar inaendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na kufanya mapitio ya baadhi ya sheria ikiwemo sheria ya maendeleo ya viwanda ambayo itawezesha wananchi kunufaika  na bidhaa zinazozalishwa viwandani.

"Kwa upande wa Zanzibar kuna jitihada kubwa zinafanyika za makusudi kwake Mhe. Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi kwa kuweka mazingira bora ya biashara na kudhibiti ushindani" alisema Mohammed Sijari Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani - ZFCC

Miongoni mwa mambo ambayo ZFCC imejifunza kutoka Tume ya Ushindani Bara ni pamoja na masuala ya ukaguzi na udhibiti wa bidhaa bandia ,taratibu za kanuni na sheria ,na masuala ya muunganiko baina ya kampuni.