Friday , 11th Mar , 2016

Kesho ndiyo kesho kwa miamba ya soka nchini Tanzania timu za Yanga na Azam na JKU zitakapokuwa katika viwanja tofauti kusaka alama tatu muhimu katika michezo ya kwanza ya hatua ya kwanza ya michuano ya vilabu barani Afrika.

Kikosi cha wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya klabu bingwa barani Afrika timu ya Yanga.

Wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya kimataifa kwa ngazi ya vilabu barani Afrika michuano ya CAF timu za Azam FC na Yanga za Tanzania bara na JKU ya Zanzibar kesho wanashuka dimbani ugenini katika viwanja tofauti kusaka alama tatu muhimu katika michezo ya kwanza ya hatua ya kwanza ya michuano ya vilabu barani Afrika.

Azam fc wao wanacheza mchezo wa kombe la shirikisho barani Afrika dhidi ya wenyeji wao timu ya Bidvest Wist ya Afrika kusini huku maafande wa jeshi la kujenga uchumi visiwani Zanzibar JKU wao watakuwa Kampala Uganda kuvaana na majogoo wa huko timu ya Sports Club Villa katika mchezo wa kombe la Shirikisho.

Yanga ambao watavaana na wenyeji wao timu ya maafande wa jeshi la Rwanda APR hiyo kesho,ambapo mkuu wa idara ya habari ya timu hiyo Jerry Muro ametamba kuvunja mwiko wa kuishia raundi za awali na kwamba wamejiwekea malengo ya kusonga hatua za juu zaidi msimu huu.

Akiongea kwa kujiamini mno Jerry Muro ambaye husifika kwa tambo nyingi za majigambo ya kusisimua hasa wanapotupiana vijembe na mkuu wa idara ya habari ya wekundu wa msimbazi Simba Haji Manara amesema mipango hiyo ya timu hiyo kuvunja rekodi si kwa maneno bali ni ubora wa mafiga matatu ya klabu hiyo kuanzia kikosi cha wachezaji bora na benchi bora la ufundi, uongozi imara wa timu hiyo na tatu ni ushirikiano baina ya timu na umoja wa mashabiki.

Muro amesema watu wengi wamekuwa wakiibeza timu hiyo kwa kuwa mara kwa mara huhishia katika araundi za mwanzo lakini safari hii kwa mara ya kwanza anathibitisha kwa kauli yake kuwa kikosi bora walichonacho kwa sasa kikiongozwa na pacha watatu wajulikanao kama MTN akiwataja kwa mjina Msuva, Tambwe na Ngoma na wengineo wanauhakika wakuvuka raundi zote za awali na kutua katika hatua ya makundi msimu huu.

Akimalizia Jerry Muro amewaomba watanzania kuondoa tofauti zao za kiushabiki na kuelekeza dua zao zote kwa wawakilishi wote wa Tanzania katika michuano ya vilabu barani Afrika ili timu hizo ziweze kufanya vema katika michuano hiyo mikubwa barani Afrika kwa ngazi ya vilabu.