Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameitangaza siku ya Jumatano Oktoba 29, 2025 kuwa ni siku ya mapumziko ya kitaifa ili kuwawezesha Watanzania kushiriki katika shughuli ya kupiga kura.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk Moses Kusiluka imebainisha kuwa uamuzi huo umetolewa baada ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kutangaza siku hiyo kuwa siku ya uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani.
“Kwa madhumuni ya kuwawezesha wananchi wenye sifa stahiki, wakiwemo watumishi wa umma na wafanyakazi wa sekta binafsi, kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura, Rais amethibitisha Oktoba 29, 2025 kuwa siku ya mapumziko,” imeeleza taarifa hiyo.
hayo nanajiri wakati ambapo Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ikiwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi siku hiyo na kutumia haki yao ya kidemokrasia kuchagua viongozi watakaowaongoza kwa miaka mitano ijayo.

