Wachezaji wa timu za Azam FC na Yanga wakikabiliana katika moja ya mchezo kati ya timu hizo.
Timu za soka za Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa ligi kuu ya soka Tanzania bara VPL baada ya kutolewa katika michuano ya klabu bingwa barani Africa na kudondokea kombe la shirikisho na Azam fc ambao nao walitolewa kombe la shirikisho wanashuka dimbani katika viwanja tofauti jijini Dar es Salaam.
Yanga wao watashuka katika dimba la taifa jijini Dar es Salaam kuwaalika maafande wa JKT Mgambo kutoka kabuku jijini Tanga katika mchezo ambao utakuwa mgumu mno kutokana na mazingira ya timu hizo ambapo Yanga wao wakiwa wanasubiri hatima ya matokeo yao ya mchezo wa nusu fainali ya kombe la shirikisho la FA ya TFF dhidi ya Coastal Union watahitaji ushindi ili kuzikimbia timu za Simba na Azam katika mbio za kuwania ubingwa huo huku Mgambo wao wakizihitaji alama tatu hizo ili kujinasua kutoka mkoani mwa ligi hiyo na kuepuka kushuka daraja.
Nao Azam kama ilivyo kwa Yanga pamoja na kutinga katika fainali ya michuano ya kombe la FA la TFF baada ya kuitoa katika michuano hiyo Mwadui FC kwa mikwaju ya Penati 5-3 wao watakuwa na kibarua pevu kutoka kwa wanalizombe Majimaji ya Songea katika mchezo mkali utakaopigwa katika dimba la Azam Complex Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Ugumu na ukali wa mchezo huo unatokana na uwezo wa sasa wa wanalizombe majimaji wanaofundishwa na kocha Kally Ongala ambaye aliwahi kucheza na kufundisha katika kikosi cha Azam fc na huku timu hiyo ikihitaji alama tatu ili kujiwekea mazingira yakutwaa nafasi ya nne na Azam nao wakihitaji alama tatu hizo hizo ili kufufua matumaini yao katika mbio za ubingwa wa ligi hiyo.
Mpaka sasa msimamo wa ligi hiyo kwa nafasi nne za juu unaonyesha kuwa Yanga mabingwa watetezi wako kileleni kwa alama zao 59 wakifuatiwa kwa ukaribu na Simba wenye alama 57 na watatu Azam fc wenye alama 55 na ya nne wakata miwa wa Manungu Mtibwa Sugar wenye alama 43.
Na katika nafasi nne za mwisho timu zinazchungulia daraja la kwanza ni pamoja na wagosi wa kaya Coastal Union kutoka Tanga wanaoburuza mkia wakiwa na alama 22, wanaofuatia ni African Sports wenye alama 23 sawa na Mgambo ambayo kesho inacheza na Yanga, na ya nne kutoka chini ni maafande wa JKT Ruvu wenye alama 24.