Tuesday , 1st Mar , 2016

Mabondia ndugu wawili Francis na Cosmas Cheka wametoa zawadi ya ushindi wao kwa watanzania wote waliowaunga mkono na kubwa zaidi wakitaka mikanda hiyo wakamkabidha rasmi Rais John Pombe Magufuli ili kumkabidhi ushindi huo muhimu kwa watanzania.

Francis Cheka akiwa amebebwa na mashabiki mara baada ya kutangazwa mshindi.

Mabondia mabingwa wapya wa mabara na Afrika mikanda ya WBF Francis Cheka [SMG] na nduguye Cosmas Cheka hii leo wamekutana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kutoa shukrani zao kwa watanzania wote kwa kuwaunga mkono na hatimaye kutwaa mikanda hiyo ya kimataifa.

Wakiwa wameambatana na viongozi wao mabondia hao wakiongozwa na meneja wao Juma Ndambile wameahidi kuendelea kucheza kwa moyo wao wote na kulipigania taifa katika medani ya kimataifa.

Cheka amefanikiwa kuutwaa mkanda huo baada ya kumshinda bondia matata, Geard Ajetovic raia wa Serbia anayefanya kazi zake nchini Uingereza.

Katika mkutano na waandishi wa habari hii leo jijini Dar es salaam, Cheka amesema kuwa ataupeleka mkanda wake kwa Rais Magufuli kwa kuwa anataka kuongeza hamasa ya kuunga mkono mchezo wa ngumi.

“Nastahili pongezi kwa uwakilishi wangu mzuri, nimepigana na bondia mwenye kiwango cha juu kabisa na leo nimeshinda. mkanda huu ni kwa watanzania wote kama mabingwa.

"Lakini ningependa kuufikisha kwa mheshimiwa Rais Magufuli ikiwa ni sehemu ya kuonesha kwamba ninaikubali serikali yake, pia naomba iendelee kuupa mchezo wa ngumi sapoti zaidi ya hapa," alisema Cheka.

"Ilianza kwa Samatta (Mbwana) aliyetwaa uchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wa Afrika, sasa hivi ni zamu yangu. Nimeshinda mkanda wa Mabara, ni jambo la sisi watanzania kujivunia."

Hata hivyo, Cheka alikiri, mpinzani wake alikuwa na kiwango cha juu kabisa na ulikuwa upinzani mkali alioupata lakini kwa sapoti kubwa ya mashabiki wazalendo na waandishi wa habari waliojitokeza aliweza kupata nguvu na hatimaye kuibuka na ushindi huo unaomfanya sasa apate nafasi ya kupanda katika viwango vya ubora na pia kupata nafasi yakucheza pambano la kimataifa la kuwania mkanda wa dunia.