Ijumaa , 22nd Mei , 2015

Timu za Jeshi Stars na Sekondari ya Makongo za wanawake zinatarajiwa kukutana kesho katika muendelezo wa Klabu Bingwa ya Mpira wa wavu Mkoa wa Dar es salaam itakayofanyika viwanja vya shule ya msingi Uhuru wasichana jijini Dar es salaam.

Jeshi Stars inayoshikilia nafasi ya pili yenye pointi saba inashuka kuendelea kusaka pointi ili kujihakikishia inarudi katika nafasi ya kwanza ambayo mpaka sasa inashikiliwa na Tanzania Prisons yenye Pointi 11.

Kwa upande wa Timu za wanaume, Twalipo yenye pointi 14 inayoshikilia nafasi ya nne kati ya nane katika michuano hiyo, itakutana na JKT inayoshikilia nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo.

Jeshi Stars yenye pointi 20 ikiwa nafasi ya pili nyuma ya vinara wa ligi hiyo Tanzania Prisons yenye pointi 25 itakutana na Chui inayoburuza mkia katika msimamo wa ligi hiyo kwa kutokuwa na Pointi hata moja baada ya kupoteza michezo yote mpaka sasa.