Ethiopia imethibitisha mlipuko wa virusi hatari vya Marburg kusini mwa nchi jana Jumamosi, Novemba 15, kwa mujibu wa Taasisi ya Afrika ya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC).
Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) na raia wa Ethiopia, Tedros Adhanom Ghebreyesus, alithibitisha Ijumaa kwamba angalau kesi tisa ziligunduliwa kusini mwa Ethiopia, siku mbili baada ya Africa CDC kutaarifiwa kuhusu virusi vilivyoshukiwa vinavyosababisha kutokwa kwa damu katika eneo hilo.
"Ugonjwa wa virusi vya Marburg (MVD) umethibitishwa na Maabara ya Rufaa ya Kitaifa (Ethiopia)," Africa CDC ilisema.
Virusi vya Marburg ni mojawapo ya vimelea hatari sana vinavyojulikana. Kama Ebola, husababisha kuvuja damu kwa wingi, homa, kutapika na kuhara na kina kipindi cha kuingia dalili cha siku 21. Pia kama Ebola, huambukizwa kwa kugusana na viowevu vya mwili na kiwango cha vifo ni kati ya asilimia 25 na 80.
Uchunguzi zaidi wa epidemiolojia na uchambuzi wa maabara unaendelea, na aina ya virusi iliyotambuliwa inaonyesha kufanana na zile zilizotambuliwa hapo awali katika Afrika Mashariki huku mamlaka za afya za Ethiopia zikichukua hatua kwa haraka kuthibitisha na kudhibiti mlipuko katika eneo la Jinka.
Hakuna chanjo iliyothibitishwa wala tiba maalumu ya antiviral kwa ajili ya virusi vya Marburg, lakini kumwaga maji au kuingizwa kwa mshipa na kutibu dalili maalum kunaongeza nafasi za mgonjwa kuishi.
