Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amemuelezea Hayati Rais John Magufuli kuwa ni mtu mkali, ambaye hakupenda mzaha katika mambo yake.
Ayasema hayo leo katika kumbukizi ya miaka mitano ya kifo cha Hayati rais Dk.John Magufuli Machi 17 katika viwanja vya makazi yake Chato mkoani Geita, Majaliwa amewataka Watanzania kuiga mambo mazuri yaliyofanywa na kiongozi huyo.
“Yeye alikuwa ni mtu mkweli, hakuwa na mzaha katika mambo yake yaani mkali , alikemea maovu, wezi, wala rushwa, wabadhirifu wa mali za umma, na yule ambaye hakufuata misingi hii aliachana nae huo ndiyo ulikuwa utaratibu wake.
“Leo hii tunamkumbuka Hayati Magufuli, sisi ambao tulikuwa karibu naye tumeweza kushuhudia wakinufaika na busara zake, hekima zake katika kuongoza taifa hili, na kutambua rasilimali za nchi na wananchi wenyewe na wanyonge wakiwemo,” amesema Majaliwa.
Majaliwa amesema Magufuli alikuwa ni mchapakazi, mtu mwenye akili za ndani ya darasa, lakini pia hata nje ya majukumu yake, na alikuwa kiongozi mzalendo aliyejengwa na uwajibikaji, uaminifu, uadilifu na mpenda maendeleo.


