Askofu wa Kanisa la The House of Prayer International Ministry, Kanda ya Songwe na muimbaji wa nyimbo za injili, Sarah Wega, amefariki dunia baada ya Pikipiki (bodaboda) aliyokuwa akisafiria kupata ajali ya kugongwa na lori iliyotokea Machi 16, 2026 katika eneo la Chapwa, Wilaya ya Momba mkoani Songwe.
Kwa mujibu wa taarifa za tukio hilo, marehemu alipata ajali akiwa kwenye usafiri wa bodaboda akielekea kijiji cha Chiwezi kwa lengo la kumtembelea ndugu yake ambaye alipata ajali.
Katika ajali hiyo, dereva wa bodaboda ambaye jina lake halijafahamika alifariki papo hapo, huku Askofu Sarah akifariki dunia baadaye alipokuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe.
Kaka wa marehemu, Michael Wega, amesema alipokea taarifa za ajali hiyo majira ya saa 3:00 usiku wa Machi 16, 2026.
“Nilipata taarifa kuwa mdogo wangu amepata ajali eneo la Chapwa akiwa kwenye bodaboda baada ya kugongwa na lori. Dereva wa bodaboda alifariki papo hapo, lakini mdogo wangu alifariki baada ya kufikishwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, baada ya kupatiwa matibabu ya awali katika Kituo cha Afya Chapwa,” ameeleza.
Kwa upande wake, msemaji wa kanisa hilo, Gervasi Mwanyula, ambaye pia ni msaidizi wa Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Furaha Mwakabenga, amesema kanisa limepokea tukio hilo kwa masikitiko makubwa.


