Jumapili , 16th Nov , 2025

“Ni wajibu wetu wote kuendelea kumtanguliza Mungu na kuiombea nchi yetu ili iendelee kuwa na amani,” amesisitiza Dkt. Nchemba.

Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amewasilisha salamu za Rais Samia Suluhu Hassan aliposhiriki ibada na waumini na viongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kisasa mkoani Dodoma akiwasisitiza Watanzania kuendelea kuliombea Taifa ili kudumisha amani, upendo, ustahimilivu na mshikamano.

Dkt. Mwigulu alitoa kauli hiyo leo Jumapili, Novemba 16, 2025 na kusisitiza kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kuhakikisha amani inaendelea kulindwa na kuenziwa, kwani bila amani, Taifa haliwezi kutekeleza majukumu yake, ikiwemo kuendesha ibada na shughuli nyingine za kijamii.

“Mhe. Rais anawasalimu sana. Yuko pamoja nanyi, na rai yake kwa Watanzania wote ni kuendeleza maombi kwa Taifa letu, kuwa watulivu na kuiombea amani iendelee kudumu,” amesema Waziri Mkuu wakati akitoa salamu hizo kwa waumini wa kanisa hilo.

“Pasipo amani hatuwezi kutekeleza majukumu mengine yeyote, hatuwezi kuendesha ibada. Hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kuiombea nchi yetu, pakiwa na amani tunaweza kutekeleza yale yaliyo katika matarajio yetu, hata kutatua yale tunayoyaona kuwa ni magumu,” Ameongeza.

“Ni wajibu wetu wote kuendelea kumtanguliza Mungu na kuiombea nchi yetu ili iendelee kuwa na amani,” amesisitiza Dkt. Nchemba.

katika Ibada hiyo iliyoongozwa na Askofu wa KKKT Dayosisi ya Dodoma, Dkt. Christian Ndossa, Dkt. Mwigulu ameambatana na Mwenza wake, Mama Neema Mwigulu Nchemba, katika ibada hiyo.

Viongozi wengine waliohudhuria ibada hiyo ni pamoja na Naibu Spika wa Bunge, Daniel Sillo, Mbunge wa Kilolo, Ritha Kabati, Mbunge wa Simanjiro, James Ole Millya, Mbunge wa Viti Maalumu, Balozi Dkt. Pindi Chana, Mbunge wa Itigi, Yohana Msita na Mbunge wa Kalenga, Jackson Kiswaga.