Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi ameondoka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa N’djili, Kinshasa mara baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Tisa wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR), uliyofanyika, Jijini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Dkt. Nchimbi alikwenda nchini Congo (DRC) juzi Ijumaa kumwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika Mkutano huo wa tisa wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Nchi za Maziwa Makuu uliofanyika Jumamosi, Novemba 15, 2025 jijini Kinshasa.
Mkutano huo ambao ulitanguliwa na vikao vya Wataalam, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi pamoja na Kamati za Mawaziri wa Kisekta, ikiwemo Ulinzi, Madini na Jinsia, umebebwa na kauli mbiu ya “Uimarishaji wa Amani na Usalama kwa Maendeleo Endelevu katika Eneo la Maziwa Makuu”
Kupitia kaulimbiu hiyo, nchi wanachama zimejadili hali ya usalama katika Ukanda wa Maziwa Makuu na kupendekeza njia za kuimarisha amani na usalama kwenye eneo hilo.
Katika Mkutano huo, Tanzania iliunga mkono ajenda zote muhimu zilizojadiliwa ikiwemo ya amani na usalama na kusisitiza kuwa itaendelea kutoa mchango mkubwa kama inavyofanya katika nchi mbalimbali kuhakikisha kuwa amani ya kweli inapatikana kwenye Kanda hiyo.
