Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba na Waziri wa Fedha Dkt Mwigulu Nchemba
Gavana Tutuba amesema hayo wakati akimkabidhi Dkt. Nchemba, noti kifani za shilingi elfu 10, elfu tano, elfu mbili na shilingi elfu moja, katika ofisi ndogo za Wizara ya Fedha, Jijini Dar es Salaam, kwa mujibu wa sheria na taratibu zinazosimamia masuala ya fedha nchini.
"Mheshimiwa Waziri, ninayo furaha kukujulisha kuwa zoezi letu la uchapaji upya wa noti kwa marejeo ya toleo la mwaka 2010, limekamilika na tayari tumewajulisha wananchi kupitia taarifa niliyoitoa kupitia Gazeti la Serikali," amesema Gavana Tutuba.
Gavana Tutuba alifafanua kuwa noti hizo zitatumika sambamba na noti zilizopo hivi sasa, zinamwonekano wa noti zinazotumika hivi sasa zilizotolewa mwaka 2010, ikiwemo alama za usalama, ukubwa, rangi na mambo mengine, isipokuwa ina marekebisho kwenye saini ya Waziri wa Fedha, na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania.
"Saini ya aliyekuwa Waziri wa Fedha ambaye hivi sasa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango imebadilishwa na kuwekwa Saini yako Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na Saini ya aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania aliyestaafu, Prof. Florens Luoga, imebadilishwa na kuwekwa Saini ya Gavana wa Benki Kuu wa sasa, Bw. Emmanuel Tutuba," ameongeza
Akizungumza baada ya kupokea sampuli za noti hizo mpya, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, alimshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu jambo hilo kufanyika na kumpongeza Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba, kwa kusimamia mchakato wa uchapaji wa noti hizo kwa weledi na uadilifu mkubwa.