Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri
Wito huo umetolewa na Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri, wakati anaongea na EATV kuhusu uwekezaji wa hati fungani.
"Nawashauri sana watanzania kupatabtaaifa sahihi kutoka kwenye kampuni sahihi, ikiwezekana waende kabisa kwenye ofisi, kupata taarifa kamili kabla ya kuwekeza sasa hivi kumekuwa na wimbi jingine la makampuni ya kuwekeza aina ya uwekezaji ambao sio salama, kwahiyo hili waswahili tunasema macho kumkichwa, kwamba uwe makini na baadhi ya uwekezaji , tujiridhishe, nenda tembelea, nenda kwenye ofisi zao lakini nenda kwenye mamlaka, unaweza kuja kituo cha uwekezaji, lakini ipo mamlaka inayosimamia inaitwa CMSA, lakini unaweza kuja kwenye soko la hisa ukauliza kuna hawa mabwana wanaitwa fulani je wapo, mnawafahamu na ukawekeza", Gilead Teri, Mtendaji Mkuu TIC.
Kuhusu uwekezaji wa masoko ya fedha (iTrust), Teri amesisitiza umuhimu wake, akieleza kuwa ili uwekezaji wa kawaida ukue, ni lazima kuwe na fedha za kutosha kwenye uchumi. Uwekezaji huu wa iTrust unaleta fedha muhimu zinazosaidia ukuaji wa uchumi.
Mwakilishi kutoka kampuni ya I TRUST, Profesa Mohamed Wasame, anaelezea umuhimu wa wananchi kuwekeza kwenye mifuko hiyo kwa faida ya maisha ya sasa na baadae.
"Tumeweza kuwapa fursa watanzania wote kila mmoja kwa uwezo wake, aje awekeze katika hii mifuko mitano ambayo tumezindua leo, kwahiyo faida ya mifuko ni nini yule meneja wenu, ambaye atakuwa anachukua i trust kwenu na anakuwa anaweza kuwekeza hisa katika hati fungani, katika mitaji yote kwenye soko la mitaji ya Tanzania akawaongezea faida wale wawekezaji, kwahiyo unaweza ukawa unapata faida ambayo ni zaidi ya ukiweka tu hela yako ikae bila kufanyia chochote", PROF.MOHAMED WASAME-Mwakilishi I Trust.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, CPA Nicodemus Mkama, alieleza kuwa kuanzishwa kwa mifuko hii ni hatua muhimu katika juhudi za serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi kote nchini, ikiwa ni pamoja na vijijini, ili kuwasaidia kiuchumi.
Mkama alisema mauzo ya awali ya vipande vya uwekezaji katika mifuko hii yalianza tarehe 12 Novemba 2024, na kampuni inatarajia kukusanya jumla ya shilingi bilioni 37.
Alisema Fedha hizo zitawekezwa katika masoko ya fedha na mitaji, ikijumuisha hisa za kampuni zilizoorodheshwa kwenye Soko la Hisa, hatifungani za serikali, hatifungani za kampuni, na dhamana za serikali za muda mfupi.
“Lengo la uwekezaji wa aina hii ni kuifanya mifuko kuwa na ukwasi unaotosha ili kukidhi mahitaji ya fedha za wawekezaji pindi mahitaji yanapotokea. Aidha, kwa upande wa mfuko wa Imaan, fedha zitakazopatikana zitawekezwa kwenye bidhaa za masoko ya mitaji zinazozingatia misingi ya Sheria, ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika hatifungani", CPA Nicodemus Mkama, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana.