Ijumaa , 2nd Mei , 2014

HOTUBA YA MHESHIMIWA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE KWENYE KILELE CHA SIKUKUU YA WAFANYAKAZI DUNIANI,
MEI MOSI 2014, DAR ES SALAAM.

Rais Kikwete akihutubia watanzania katika Sherehe za siku ya wafanyakazi duniani Mei Mosi

HOTUBA YA MHESHIMIWA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE KWENYE KILELE CHA SIKUKUU YA WAFANYAKAZI DUNIANI,
MEI MOSI 2014, DAR ES SALAAM

Kaimu Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania;
Bibi Northburga Maskini;
Waziri wa Kazi na Ajira, Mheshimiwa Gaudensia Mugosi Kabaka(MB);
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi,
Mh. Regina Rweyemamu;
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Sadiki
Meck Sadiki;
Waheshimiwa Mawaziri na Wabunge;
Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Dunia (ILO), Kanda ya
Afrika Mashariki, Ndugu Alexio Msindo;
Viongozi mbalimbali wa Serikali mliopo hapa;
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi,
Ndugu Nicholaus Mgaya;
Ndugu Almas Maige, Mwenyekiti wa ATE;
Mkurugenzi Mtendaji, Chama cha Waajiri Tanzania (ATE),
Dr. Aggrey Mlimuka;
Mheshimiwa Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM na Viongozi wa Vyama vya Siasa Mliopo;
Waheshimiwa Mabalozi;
Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri, Ndugu Doroth Uiso;
Wenyeviti na Makatibu wa Vyama vya Wafanyakazi;
Viongozi wa Vyama vya Siasa;
Ndugu Wafanyakazi wenzangu;
Mabibi na Mabwana;
Shukrani
Awali ya yote naomba tuanze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kutujalia uhai na kutuwezesha kukutana leo katika sherehe za mwaka huu za kuadhimisha siku ya wafanyakazi duniani. Aidha, natoa shukrani nyingi kwa Kaimu Rais wa TUCTA Mama Northburga Maskini na viongozi wenzako kwa heshima kubwa mliyonipa ya kuja kuungana na wafanyakazi wa Tanzania katika kuadhimisha siku hii adhimu.
Napenda kutumia fursa hii kupitia kwako Kaimu Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania, kutoa salamu nyingi za pongezi na mkono wa heri kwa wanachama na Viongozi wa Vyama Vyote vya Wafanyakazi katika kuadhimisha siku hii kubwa na adhimu. Nawapongeza sana Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Habari na Utafiti (RAAWU) kwa kuratibu vizuri maadhimisho ya mwaka huu. Nimefurahi kusikia kuwa maadhimisho ya mwaka huu yamehusisha wiki ya wafanyakazi ambako kumekuwa na maonyesho ya waajiri na wafanyakazi. Huu ni utaratibu mzuri ambao licha ya kuongeza hamasa kwa maadhimisho haya lakini pia umetoa fursa kwa wananchi wengi kujionea wenyewe mambo muhimu mnayoyafanya wafanyakazi.
Nitakuwa mwizi wa fadhila nisipowapongeza na kuwashukuru wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Saidi Meck Sadiki kwa kukubali kuwa wenyeji wa sherehe hii. Si kazi rahisi hata kidogo, hivyo wanastahili pongezi zetu kwa kufanikisha vyema shughuli hii. Tumeona jinsi uwanja ulivyofurika na maandamano yalivyofana. Usione vinaelea vimeundwa. Tafadhali pokeeni pongezi zetu sote.

Pongezi kwa Wafanyakazi Bora
Wafanyakazi Wenzangu,
Kwa mara nyingine tena katika sherehe hizi wafanyakazi bora wametambuliwa na kupewa tuzo. Mnastahili pongezi zetu sote kwa kufanya kazi kwa bidii, maarifa na nidhamu na kutambuliwa. Wahenga walisema, ”Chanda chema huvishwa pete”. Nawapongeza TUCTA na waajiri kwa kutambua umuhimu wa kutoa tuzo kwa wafanyakazi bora. Inaongeza ari ya kufanya kazi na tija kazini. Tafadhali udumisheni utaratibu huu. Kwa wale ambao hawakupata safari hii wasikate tamaa na wao siku yao yaja waongeze bidii, maarifa na nidhamu kazini ili mwakani, siku kama ya leo iwe zamu yao kupongezwa.
Risala ya Wafanyakazi
Ndugu Kaimu Rais wa TUCTA,
Wafanyakazi Wenzangu,
Nimeisikiliza kwa makini sana risala yenu iliyowasilishwa na Katibu Mkuu wa TUCTA Ndugu Nicholas Mgaya ambaye anastahili pongezi kwa kuwasilisha vizuri na kueleweka. Ni risala nzuri iliyosheheni mawazo mazuri ya kujenga. Ndani yake inayo maombi, lakini pia mapendekezo. Napenda kuwahakikishia kuwa mapendekezo yote nimeyachukua na tutakwenda kuyafanyia kazi. Baadhi ya maombi si mapya, yamerudiwa ili kuweka msisitizo. Mengine majawabu yake tunayo, nitayatolea maelezo katika hotuba yangu.
Kauli Mbiu
Wafanyakazi Wenzangu,
Nawapongeza kwa Kauli mbiu yenu isemayo, ”Utawala Bora Utumike Kuondoa Kero za Wafanyakazi”. Kauli mbiu hii ni muafaka na maridhawa kabisa. Ni ukweli usiopingika kuwa utawala bora ni jambo muhimu sana na pale ambapo upo si tu kwamba husaidia kutatua kero za wafanyakazi, bali pia huepusha mikwaruzano na migogoro kati ya wafanyakazi na waajiri.
Wafanyakazi Wenzangu,
Uzoefu unaonyesha kuwa migogoro ya wafanyakazi na waajiri hujitokeza zaidi pale ambapo kanuni za utawala bora za ushirikishwaji, uwajibikaji na uwazi hazifuatwi. Usiri usiyo wa lazima katika uamuzi, hufanya hata uamuzi mzuri kutiliwa shaka na kujenga hofu isiyostahili kuwepo. Wakati mwingine inaweza kusababisha hata uamuzi mzuri kukataliwa. Pia, ukosefu wa taarifa sahihi unaweza kusababisha wafanyakazi kutoa madai yasiyotekelezeka kwa sababu ya kuwa na matarajio makubwa mno kuliko uwezo wa mwajiri kumudu.
Tumejifunza, vilevile, kuwa utawala bora hauishii kwenye kutunga sheria na kuunda taasisi na vyombo vya usimamiaji na utekelezaji wa Sheria. Utawala bora hauna budi kuwa sehemu kamili ya utamaduni wa kazi na uhusiano ambao unapaswa kuzingatiwa na waajiri na waajiriwa. Wakati mwajiri anawajibika kuwa muwazi kwa wafanyakazi wake na kuwatimizia stahili zao kama inavyopasika, waajiriwa nao wanawajibika kumtendea haki mwajiri kwa kufanya kazi kwa bidii na kuheshimu taratibu za kazi ikiwa ni pamoja na zile zihusuzo namna ya kuwasilisha madai yao.
Waajiri na waajiriwa kudai haki zao hakuwaondolei wajibu wao kwa kila mmoja wao. Hivyo basi, kudumisha utawala bora kunawataka waajiri na wafanyakazi kuheshimu Sheria za nchi zikiwemo zile zinazotawala uhusiano na ajira sehemu za kazi. Hapa nazungumzia, Sheria ya Majadiliano katika Utumishi wa Umma ya Mwaka 2003 na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya Mwaka 2004.
Ndugu Zangu;
Lazima tutambue na kukubali kuwa ufanisi sehemu za kazi hutegemea uhusiano uliopo baina ya wafanyakazi na waajiri. Kama umejengwa juu ya misingi ya kuheshimu sheria na majadiliano, mambo huwa mazuri. Vitisho vya mwajiri na migomo ya wafanyakazi si suluhisho la kuondoa kero za wafanyakazi. Kwa jumla hupunguza ufanisi. Hivyo basi, lazima tufanye kila tuwezalo kujenga uhusiano mwema kati ya waajiri na waajiriwa. Ni kichocheo kikubwa cha watu kufanya kazi kwa bidii, kuongeza tija na uzalishaji sehemu za kazi hivyo kumwongezea mwajiri kipato na uwezo wa kuboresha maslahi ya wafanyakazi.
Hali ya Uchumi
Ndugu Viongozi na Ndugu Wafanyakazi;
Mwenendo wa uchumi wetu katika mwaka 2013/2014 ni mzuri. Uchumi umeendelea kuimarika ikilinganishwa na mwaka uliopita. Ukuaji wa uchumi unategemewa kuongezeka kutoka asilimia 7.0 ya mwaka 2013 hadi asilimia 7.2 mwaka huu. Haya ni matunda ya kazi nzuri ya wafanyakazi, wakulima na wadau wengine nchini. Tunayo kila sababu ya kujipongeza kwa mafanikio haya.
Habari nyingine njema kwa wafanyakazi ni kwamba mfumuko wa bei umeteremka kutoka asilimia 9 tulipokutana mwaka jana hadi asilimia 6.3 tunapokutana leo. Azma yetu ni kutaka ubaki chini ya asilimia 10 na hasa uwe asilimia 5 au chini ya hapo ifikapo Juni, 2015. Tunahangaikia sana kushuka kwa mfumuko wa bei kwa vile unapokua juu, unasababisha hali ngumu ya maisha kwa wafanyakazi. Tukidhibiti mfumuko wa bei uongezaji wa viwango vya mishahara utakuwa na tija. Aidha, inamuwezesha hata yule mwenye mshahara mdogo kuweza kukidhi baadhi ya mahitaji yake muhimu, hivyo kumpunguzia ukali wa maisha. Kwa sababu hiyo, hatuna budi kuongeza bidii katika kukuza uchumi na kushusha mfumuko wa bei. Kwa vile hapa tulipofika sio ukomo wa uwezo wetu, naamini tunaweza kupata mafanikio makubwa zaidi tukiongeza utawala bora mahala pa kazi. Kiwango cha ukuaji wa uchumi kinaweza kuwa kikubwa zaidi na kutunufaisha sote.

Mabaraza ya Wafanyakazi
Ndugu Wafanyakazi;
Hatuwezi kuzungumzia utawala bora mahala pa kazi bila ya kuwa na ushirikishwaji wa wafanyakazi. Ushirikishwaji wa wafanyakazi, unawezekana tu pale ambapo yapo mabaraza ya kazi na yanafanya kazi. Mabaraza ya kazi ni fursa kwa wafanyakazi kuwakilisha na kujenga madaraja kati ya menejimenti na wafanyakazi. Madaraja haya hujenga mazingira ya kuwezesha madai ya wafanyakazi kufika katika menejimenti, na uamuzi kufanywa na mrejesho wa menejimenti kuwafikia wafanyakazi.
Nimepata taarifa isiyofurahisha kuwa bado zipo taasisi chache za Serikali ambazo hazijaunda mabaraza hayo. Nimeambiwa pia kwamba baadhi ya yale mabaraza yaliyoundwa hayakutani kama inavyopasa. Hata hawakutani kujadili bajeti za taasisi zao, jambo ambalo ni sharti la msingi kutekelezwa kwa kisingizio cha kukosa fedha. Madai haya hayaingii akilini hata kidogo. Mbona semina na vikao vya menejimenti vyenye posho nono hatuoni vikiachwa kufanyika?.
Napenda kuwakumbusha wakuu wa taasisi zote za umma kuwa uundwaji mabaraza ya wafanyakazi na ushirikishwaji wa mabaraza hayo katika mchakato wa Bajeti sio jambo la hiari bali ni matakwa ya kisheria. Wasiounda mabaraza na wale wasioitisha vikao vya mabaraza kujadili bajeti za taasisi zao wanavunja sheria. Hili ni jambo lisilovumilika. Nimewaagiza Waziri wa Kazi na Ajira na Katibu Mkuu Kiongozi wahakikishe kuwa Wizara zote na taasisi zote za umma zinazingatia Agizo la Rais Na. 1 la Mwaka 1970 pamoja na matakwa ya Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na.6 ya Mwaka 2004. Lazima wahakikishe kuwa mabaraza yanaundwa mapema iwezekanavyo, na zile Wizara, Idara na Taasisi zisizoitisha mabaraza yao zibanwe kufanya hivyo bila ajizi.
Umuhimu wa Vyama vya Wafanyakazi Mahali pa Kazi
Ndugu Wafanyakazi;
Jambo lingine ambalo limenisikitisha sana ni taarifa kuwa bado wapo waajiri hasa katika sekta binafsi ambao wanakaidi matakwa ya kisheria ya kuwepo kwa matawi ya vyama vya wafanyakazi mahala pa kazi. Naambiwa hata pale wafanyakazi wanapoanzisha mabaraza hayo, wale wafanyakazi wanaokuwa mstari wa mbele kudai kuwepo matawi hayo au kutetea haki za wafanyakazi wamekuwa wanapata wakati mgumu. Huishia kuhamishwa au hata kufukuzwa kazi. Aidha, wapo baadhi ya waajiri ambao wameanzisha mifumo mbadala ambayo haiko kisheria katika kukwepa kushughulikia maslahi ya wafanyakazi.
Napenda kurudia na kusisitiza kuwa kuwepo kwa matawi ya vyama vya wafanyakazi mahala pa kazi si suala la hiyari bali ni matakwa ya kisheria. Hivyo, hakuna sekta, kampuni wala mwekezaji ambaye yuko juu ya sheria hii. Ni vizui ukaeleweka kuwa hii si tu ni sheria ya nchi yetu peke yake, bali ni matokeo ya mikataba ya kimataifa na ni haki ya msingi ya wafanyakazi na utawala bora.
Ndugu Viongozi na Ndugu Wafanyakazi;
Sisi katika Serikali ni mashahidi wa manufaa ya kuwepo kwa matawi ya wafanyakazi mahala pa kazi. Uzoefu wetu umetuthibitishia kuwa pale ambapo kuna matawi ya vyama vya wafanyakazi ambayo yanatimiza majukumu yake vizuri na menejimenti inatimiza wajibu wake ipasavyo uhusiano wa kikazi huwa mzuri. Inasaidia kupunguza migogoro, kuepusha migomo na huongeza tija na ufanisi. Matawi hayo hutoa fursa ya majadiliano na mazungumzo kati ya wafanyakazi na waajiri. Si kweli hata kidogo kuwa, kuwepo kwa matawi haya hukwamisha ufanisi mahala pa kazi.
Nimemwagiza Waziri wa Kazi kuhakikisha kuwa matawi ya vyama vya wafanyakazi yanakuwepo mahala pa kazi. Pia, ahakikishe kuwa wakaguzi wanapita sehemu za kazi na kukagua utekelezaji wa sheria kuhusu kuwepo kwa matawi hayo. Wale waajiri wanaokaidi wachukuliwe hatua za kisheria bila kuoneana muhali. Aidha, nimemtaka asisite kuwachukulia hatua zipasazo za kinidhamu, wakaguzi wanaoshirikiana na waajiri kudhoofisha haki za wafanyakazi. Hawa ni watu walioshindwa kutimiza majukumu yao hivyo wasivumiliwe. Wanaipaka matope Serikali.
Wapo Wakaguzi ambao wanakwazwa na kukaa kituo kimoja kwa muda mrefu, wamezoeleka mno na wamejenga mazoea yasiyofaa kati yao na waajiri na wanashirikiana kuwakandamiza wafanyakazi. Wahamishwe. Wakati huohuo wakumbusheni kuwa kazi yao ni kusimamia sheria, kutetea haki za wafanyakazi na waajiri na kamwe sio kuwa mawakala wa kuwasaidia waajiri kukiuka sheria.
Hatua za Serikali dhidi ya Uwakala wa Ajira
Ndugu Wafanyakazi;
Nimefurahishwa sana na uamuzi wa Mheshimiwa Gaudensia Kabaka, Waziri wa Kazi na Ajira na viongozi wenzake Wizarani wa kufuta mfumo mpya ulioanzishwa wa makampuni kuajiri kupitia uwakala wa ajira. Naunga mkono uamuzi wenu wa kupiga marufuku utaratibu unaofanywa na baadhi ya Wakala Binafsi wa Huduma za Ajira nchini wa kukodisha wafanyakazi katika Makampuni. Utaratibu huu ni kinyume cha Sheria ya Huduma za Ajira Na. 9 ya 1999. Sheria ya Huduma ya Ajira inaelezea majukumu ya msingi ya Wakala Binafsi wa Huduma za Ajira kuwa ni kuwaunganisha watafuta kazi na waajiri na siyo wao kuwa waajiri na kukodisha wafanyakazi kwa makampuni.
Wakala wa Ajira kufanya mambo kinyume na matakwa ya sheria haikubaliki. Anawakosesha wafanyakazi haki zao za msingi kama vile mishahara, huduma za hifadhi ya jamii, likizo ya uzazi, matibabu, mafunzo na mengineyo. Inaondoa uwajibikaji wa moja kwa moja wa waajiri kwa wafanyakazi wao. Hili ni jambo ambalo hatuwezi kuliacha liendelee. Nimempa Waziri wa Kazi na Ajira baraka zangu zote kulishughulikia kwa nguvu zake zote na kwa umakini na ufanisi mkubwa ili tuweze kukomesha kabisa dhulma hii.
Uimarishaji wa Vyombo vya Mashauriano
Wafanyakazi wenzangu;
Jambo lingine ambalo linahitaji kupatiwa ufumbuzi katika kuimarisha uhusiano kati ya wafanyakazi na waajiri ni ufanisi wa vyombo vya mashauriano. Serikali imefanya kazi nzuri ya kuunda vyombo hivi ikiwemo Baraza la Mashauriano (LESCO). Lengo la kuunda mabaraza hayo ni kutoa fursa ya usuluhishi wa migogoro ya kikazi na maslahi ya wafanyakazi kabla ya kuiwasilisha katika mifumo ya kimahakama.
Pamoja na nia njema ya Serikali, chombo hiki kimeendelea kulalamikiwa kwamba hakitekelezi wajibu wake kwa ukamilifu. Mashauri yanayowasilishwa hayatatuliwi kwa wakati kutokana na Baraza hili kutoitisha vikao, kwa madai ya ufinyu wa bajeti. Matokeo yake, wafanyakazi aidha wanaamua kufikisha migogoro yao kwa Waziri wa Kazi, au kwenda mahakamani au kuchukua sheria mkononi. Hatua zote hizi nje ya matumizi ya Baraza la LESCO, si endelevu na hazijengi mazingira ya maridhiano kati ya waajiri na wafanyakazi. Kwa jumla zinadhoofisha utawala bora.
Nimeelekeza, kuanzia bajeti ya mwaka wa fedha 2014/2015, Wizara ihakikishe inatenga fedha za kutosha za kuwezesha Baraza la LESCO kufanya vikao vyake. Aidha, bajeti hiyo ilindwe ili kuhakikisha kuwa pesa hizo zinatumika kwa ajili ya kazi za Baraza la Mashauriano. Ni jambo linalowezekana. Nataka tuone kuwa kuanzia mwaka ujao wa fedha Baraza hili linafanya kazi yake ipasavyo. Sote tunakubaliana kuhusu umuhimu wake kuwa ni mkubwa na ipo mifano ya nchi nyingine ambazo Baraza hili hufanya kazi kwa ufanisi mkubwa.
Naamini kwamba, kwa kuwa changamoto yetu si udhaifu wa Sheria yenyewe iliyounda LESCO bali ufanisi katika utendaji tu, upatikanaji wa fedha za kutosha utawezesha Baraza hili kufanya kazi kwa ufanisi. Mwisho wa yote tutaepusha migogoro isiyo ya lazima, lakini pia tutaimarisha utawala bora kwa kujenga madaraja kati ya watumishi na waajiri pale panapojitokeza mikwaruzano.
Ushiriki wa Wafanyakazi kwenye Bodi za Mashirika
Wafanyakazi Wenzangu,
Sambamba na kulihuisha Baraza la LESCO, Serikali inalifanyia kazi suala la kushirikisha wafanyakazi katika Bodi za Mashirika ya Umma. Tunafanya hivyo kwa kutambua kuwa, Bodi za Mashirika ni vyombo muhimu vinavyofanya uamuzi wa kisera na kiuendeshaji wa mashirika. Uamuzi wake hugusa moja kwa moja maslahi ya wafanyakazi hivyo uwakilishi wao ni muhimu.
Natambua kuwa tayari yapo mashirika ambayo kwa mujibu wa Sheria ya kuanzishwa kwake, yametambua uwakilishi wa wafanyakazi katika Bodi zake. Lakini yapo mashirika mengine hayana sharti hilo katika Sheria zilizounda mashirika hayo. Manufaa na umuhimu wa kuwashirikisha wafanyakazi si mambo yanahotaji mjadala. Yapo wazi. Katika yale mashirika ambayo Bodi zake zina wajumbe kutoka vyama vya wafanyakazi, tumeona namna ambavyo mchango wa wafanyakazi umekuwa wa msaada mkubwa.
Nimeelekeza Wizara husika na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuchukua hatua za haraka kuandaa na kuwasilisha muswada wa Sheria Bungeni wa kulirasimisha jambo hili kwa mashirika yote ya umma. Lengo letu ni kutaka kuhakikisha kuwa, jambo hili muhimu haliwi suala la utashi tu wa Shirika husika, bali ni utaratibu rasmi wa kisheria. Naamini ushiriki wa wafanyakazi katika Bodi za Mashirika utaimarisha utawala bora na kupunguza kero za wafanyakazi mahala pa kazi.
Maslahi ya Wafanyakazi
Ndugu Kaimu Rais, Ndugu Viongozi na Ndugu Wafanyakazi;
Nafahamu kuwa hotuba yangu haitakuwa imekamilika bila kuzungumzia maslahi ya wafanyakazi. Na, wengi hasa wanasubiri kusikia nasema nini kuhusu nyongeza ya kima cha chini cha mshahara na kupungua kwa kodi ya mapato, yaani Paye As You Earn (P.A.Y.E).
Napenda kurudia kuwahakikishia kuwa mimi na wenzangu Serikalini hatuna upungufu wa dhamira ya kufanya hivyo. Tumethibitisha hivyo miaka iliyopita na tutaendelea kuwa hivyo. Leo nitapenda kuzungumzia mambo matatu: La kwanza ni kuhusu Kima cha Chini cha Mshahara. Kama tulivyoahidi mwaka jana, Serikali ilipandisha kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa Umma kwa asilimia 41. Kwa ongezeko hilo, kima cha chini cha watumishi wa umma kiliongezeka kutoka shilingi 170,000 hadi shilingi 240,000. Na mwaka huu nawaahidi tena kuwa tutaongeza. Najua kwamba nyongeza hii si kubwa kuliko vile ambavyo wafanyakazi na hata mimi ningependelea iwe. Kwa kweli kinachotukwaza ni mapato ya Serikali kutokuwa makubwa kumudu nyongeza kubwa ya mshahara kwa wakati. Nyongeza hii peke yake inaifanya Serikali kutumia asilimia 44.9 ya bajeti ya Serikali kulipa mishahara na asilimia 10 ya pato la taifa (GDP). Kwa vigezo vyo vyote vile kiwango hiki ni kikubwa mno hivyo ni kielelezo thabiti cha dhamira yetu njema na kujali.
Isitoshe naomba mkumbuke kuwa mwaka 2005 kima cha chini cha mshahara kilikuwa shilingi 65,000.00. Hivyo ndani ya miaka saba tumeongeza kima cha chini karibu mara nne ya ilivyokuwa na kufikia kima cha chini cha sasa. Nawaahidi mwaka huu tutaongeza tena. Kama nilivyogusia, hatuwezi kutoa nyongeza kubwa mara moja lakini, kidogo kidogo tunaweza. Na tumeweza. Naamini, miaka mitano ijayo mambo yatakuwa mazuri zaidi wakati mapato ya Serikali yatakapoongezeka sana mauzo ya gesi asilia yatakapoanza.
La pili ni Kima cha Mishahara Katika Sekta Binafsi: Kima cha chini cha mishahara katika sekta binafsi bado hakinifurahishi. Kwa upande wa sekta binafsi, mfumo wa upangaji wa kima cha chini cha mshahara unatawaliwa na Sheria ya Taasisi za Kazi Na. 7 ya Mwaka 2004. Sheria hii inaanzisha Bodi za Mishahara za kisekta ambazo zina wajibu wa kutoa mapendekezo kwa Waziri wa Kazi na Ajira kuhusu kima cha chini cha mshahara katika sekta husika. Naambiwa kuwa Bodi hizi zinapata changamoto katika utekelezaji wa majukumu yake kwa kuwa waajiri hawatoi ushirikiano wa kutosha.
Mnamo mwezi Juni, 2013, Mhe. Waziri wa Kazi na Ajira alitangaza mishahara ya kima cha chini kisekta kupitia Gazeti la Serikali Na. 196/2013 kwa sekta 12 za Madini, Afya, Kilimo, Nishati, Usafirishaji, Viwanda, Ujenzi, Ulinzi binafsi, Shule binafsi, Hoteli, Huduma za Majumbani na Mawasiliano. Taarifa ninayopata ni kuwa, sehemu kubwa ya waajiri wa sekta binafsi hawazingatii viwango hivyo. Nimemuelekeza Waziri wa Kazi awabane wsiotekeleza watekeleze Tuzo alizotoa.
Naguswa sana na kilio cha wafanyakazi katika sekta binafsi. Sisi kama Serikali hatuwezi kukwepa wajibu wa kuwasaidia. Nimeelekeza kuwepo na mkakati maalum kushughulikia jambo hili. Katika mkakati huo, nashauri utaratibu wa Utatu yaani Wafanyakazi, Waajiri na Serikali utumike kufanya tathmini na kubaini matatizo yaliyopo na kupendekeza namna bora ya kuhakikisha wafanyakazi wa sekta binafsi wanapata mishahara wanayostahili. Katika mkakati wa muda mrefu, tumekubaliana na viongozi wenu kuimarisha vyombo vya mashauriano, usimamizi na bodi za kisekta ili huko mbele ya safari visimamie kwa ukamilifu jambo hili.
Jambo la tatu ni Kodi ya Mapato kwa wafanyakazi yaani PAYE: Kumekuwepo pia na ombi la muda mrefu la kupunguza kodi inayokatwa kwenye mishahara ya wafanyakazi kuwa chini ya asilimia 10. Kama nilivyoahidi mwaka jana, hili tutaendelea kulishughulikia kadri uwezo wa Serikali utakaporuhusu. Tumeshafanya hivyo kabla, na hatuna sababu ya kutofanya hivyo huko tuendako. Tayari tumepunguza kutoka asilimia 18.5 mwaka 2007 hadi asilimia 13 hivi sasa. Maombi yenu tumeyapokea, tuachieni, tuangalie nini tunachoweza kufanya kama miaka iliyopita. Kwa jumla ni nia yetu kuendelea kufanya hivyo mwaka hadi mwaka, tunakwazwa na uwezo mdogo wa mapato ya Serikali.
Mageuzi katika Mifuko ya Kijamii
Wafanyakazi wenzangu;
Kama nilivyosema wakati wa sherehe za Mei Mosi zilizofanyika mkoani Mbeya mwaka jana, Serikali ina dhamira ya dhati ya kupanua wigo wa hifadhi ya jamii kwa wafanyakazi na kwa wananchi wote kwa ujumla. Hatua kwa hatua tutaendelea kufanya marekebisho katika Hifadhi ya Jamii nchini ili iweze kukidhi haja hiyo.
Eneo moja ambalo tumejiandaa kulitekeleza kuanzia Julai, 2014 ni kuhusu fidia kwa wafanyakazi wanaoumia au kuathirika wakiwa kazini. Wote tunafahamu kwamba tangu mwaka 2008 Serikali ilipitisha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi Na. 20 ambayo inaunda Mfuko wa Fidia utakaoshughulikia malipo yaliyo bora zaidi ya fidia kwa wafanyakazi wanaoumia au kufariki au kupata maradhi yatokanayo na kazi kuliko ilivyo sasa. Mfuko huu utahudumia wafanyakazi wa sekta zote yaani sekta binafsi na ya umma na utatoa mafao bora zaidi kuliko ilivyo hivi sasa.
Tunafanya hivyo kutokana na uzoefu tulioupata wa wafanyakazi wengi hasa katika sekta binafsi kushindwa kupata fidia stahili, wakati mwingine kutokana na uchanga wa waajiri wao. Kwa kuwa na mfuko huu kutawapunguzia waajiri mzigo wa kuwalipa fidia wafanyakazi wao hasa wakati ambao hawana uwezo wa kufanya hivyo. Mfuko utawapa wafanyakazi uhakika wa kulipwa fidia yao pale watakapopata madhara mahala pa kazi. Serikali itachangia asilimia moja ya jumla ya mishahara ya wafanyakazi kila mwezi kuanzia mwezi Julai, 2014. Waajiri binafsi nao watachangia asilimia 0.5 ya jumla ya mishahara ya wafanyakazi wao.
Wafanyakazi Wenzangu;
Eneo jingine ambalo tuliahidi kulifanyia kazi ni kuhusu kuainisha mafao ya pensheni. Mchakato huu unaendelea vizuri na nafahamu kuwa Mamlaka ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) na Wadau yaani Vyama vya Wafanyakazi wanatarajiwa kukutana tarehe 5 Mei, 2014 kwa majadiliano zaidi. Kikao hicho kitajadili ulingano wa mafao yanayotolewa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa kuweka vikokotoo bora vya Mafao ya Pensheni.
Ni vizuri kukumbushana kwamba, kuwa na vikokotoo vizuri ni jambo moja, na kuhakikisha uendelevu wa mifuko ya hifadhi ya jamii ni suala lingine. Hivyo, wakati tunaendelea na majadiliano hayo, hatuna budi pia kutoa umuhimu katika kuelimishana juu ya umuhimu na wajibu wa waajiri kuwasilisha michango ya wanachama. Mifuko ya hifadhi ya jamii inatakiwa kuhakikisha kuwa inakusanya michango ya wanachama wake na kuwekeza kwa umakini mkubwa. Wanachama wao wanatakiwa kuhakikisha kuwa michango yao inabaki katika mifuko ya hifadhi ya jamii ili ije kuwafaa wakati wa shida na maisha ya uzeeni, badala ya tabia ya sasa ya watumishi kuamua kushirikiana na waajiri kutokatwa michango hiyo, au kujitoa katika mifuko hiyo kila wanapobadilisha ajira kutoka kwa mwajiri mmoja kwenda kwa mwajiri mwingine.
Madai ya Waalimu
Wafanyakazi Wenzangu,
Serikali pia imeendelea kushughulikia madai mbalimbali ya watumishi wa umma hususan madeni ya mishahara na yasiyokuwa ya mishahara. Tumekamilisha uhakiki wa madeni kwa wafanyakazi wasiokuwa walimu. Hazina wameniarifu kuwa yatalipwa kabla ya mwaka ujao wa fedha. Kwa upande wa walimu, Serikali kwa kushirikiana na Chama cha Walimu (CWT) tumekuwa tunafanya uhakiki wa madeni ya walimu katika Halmashauri zote 147 za Tanzania Bara. Kazi imekamilika kwa Halmashauri 96 na inaendelea kwa Halmashauri 51 zilizosalia. Nimeambiwa kuwa madeni yaliyohakikiwa yameanza kulipwa. Na, kama nilivyosema kwa wafanyakazi wasiokuwa walimu ni makusudio ya Hazina kuwa madeni hayo yalipwe katika mwaka huu wa fedha.
Ni jambo la kutia faraja kwamba, katika kufanya kazi ya uhakiki wa madeni ya walimu. Serikali na Chama cha Walimu tumeweza kubaini mzizi wa fitina. Tumekubaliana kuutafutia dawa ya kuung’oa ili tatizo hili lisijirudie.
Kwa ajili hiyo, nimeelekeza Wizara na Taasisi zinazohusika hasa Wizara ya Fedha, Wizara ya Elimu na Mafunzo na Ufundi na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuwachukulia hatua za kisheria na kinidhamu maofisa wa Serikali, wanaohusika na udanganyifu huu. Halikadhaika, wafanyakazi walioghushi stakabadhi nao wachukuliwe hatua za kisheria. Kwa muda mrefu, udanganyifu na hila za watumishi hawa zimechochea kutokuelewana na kutokuaminiana kati ya walimu na Serikali.
Ifike mahala sasa, walimu na Serikali tupate suluhu ya kudumu baada ya kumpata mchawi wetu. Tumekubaliana kuendelea na mfumo huu wa uhakiki wa pamoja kama msingi wa kutatua tatizo hili la muda mrefu. Huu ni mfano mzuri wa namna utawala bora unavyoweza kutatua kero za wafanyakazi kupitia ushirikishaji na uwazi.
Kuhusu muundo mpya wa Utumishi wa Walimu, habari njema ni kuwa muundo huo umekwishapitishwa na unatarajiwa kuanza kutumika tarehe 1 Julai, 2014. Suala la upandishaji wa madaraja ya walimu nalo linakwenda vizuri ambapo hadi kufikia Aprili 2014, walimu 30,236 walikuwa wamepandishwa vyeo.
Kuhusu wimbo wenu, Shemeji mshahara mdogo. Nimefuatilia nimebaini ni kweli kumekuwa na ucheleweshaji. Nimefuatilia Benki Kuu wanasema walitoa pesa mapema, lakini kumekuwepo na mkwamo mahali ambapo tutapatafuta.
Utoaji Holela wa Vibali vya Ajira kwa Wageni
Ndugu Kaimu Rais wa TUCTA;
Wafanyakazi wenzangu,
Yamekuwepo malalamiko kuwa kumekuwepo na utoaji holela wa vibali vya kazi kwa wageni kufanya kazi nchini. Naambiwa siku hizi hata zile ajira ambazo Watanzania wana ujuzi nazo hujazwa na wageni. Serikali imeyafanyia kazi malalamiko haya na kugundua kuwa udhaifu upo kwenye kuwepo kwa taasisi zaidi ya moja inayoshughulika na utoaji wa vibali kwa wageni kuishi na kufanya kazi nchini. Hali hii inatoa mwanya kwa watu wasiokuwa waaminifu kutoa vibali kwa watu wasiostahili.
Serikali imeamua kuzifanyia marekebisho sheria husika na iko mbioni kuwasilisha Bungeni Muswada wa Sheria ya Vibali vya Ajira. Nimeelekeza kuwa jitihada zifanyike ili Muswada huo uwasilishe kwenye kikao cha Bunge la Oktoba, 2014. Sheria hii sasa italiweka suala la vibali vya kazi kushughuhulikiwa na taasisi moja na hivyo kuweka udhibiti katika utoaji wa vibali hivyo.
Ndugu Wafanyakazi;
Niruhusuni nichukue fursa hii, pia, kukumbusha kuhusu umuhimu wa wafanyakazi kuheshimu na kuthamini kazi. Waswahili wana msemo “Usichezee kazi, chezea mshahara”. Yapo madai yanayojirudia kutoka kwa waajiri kuwa wafanyakazi wa Kitanzania hawathamini na kuheshimu kazi zao. Wanatuhumiwa kwa uvivu, udokozi na nidhamu ndogo. Napata taabu kukubali madai haya kuwa hii ndio sifa ya wafanyakazi wote wa Kitanzania. Leo nimetunuku tuzo kwa wafanyakazi bora na tumekuwa tunafanya hivyo kila mwaka. Kitendo hiki ni ushahidi kuwa wafanyakazi hodari wapo. Hata hivyo, siwezi kusema wavivu, wezi na watovu wa nidhamu hawapo. Lakini, sina uhakika na ukweli wa madai yanayotoa sifa mbaya na kutia doa baya kwa Wafanyakazi wa Kitanzania.
Sifa hizo hasi ndizo zinazowashawishi waajiri na hasa wawekezaji kutafuta wafanyakazi nje. Ninawaomba viongozi na wanachama wa vyama vya wafanyakazi mlitafakari suala hili kwa uzito unaostahili kwani linaelekea kuaminika. Kulikataa tatizo peke yake hakutoshi kwani hakutatui tatizo lililopo, zaidi ya kutupa faraja ya muda tu. Natoa rai kwa vyama vya wafanyakazi na Wizara ya Kazi na Ajira kulifanyia kazi jambo hili haraka.
Mchakato wa Katiba
Wafanyakazi Wenzangu,
Katika sherehe za Mei Mosi zilizofanyika mwaka jana kule Mbeya, mlitoa rai ya wafanyakazi kushirikishwa katika mchakato wa kutunga Katiba Mpya. Niliwaahidi kuwa mtashirikishwa kwa vile wafanyakazi ni sehemu kubwa sana ya jamii yetu na kundi muhimu sana katika taifa. Nimetimiza ahadi yangu wakati wa kuteua Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Wajumbe 201 wa Bunge Maalum la Katiba. Kuna uwakilishi mkubwa wa wafanyakazi na kumfanya Ndugu Maige, Mwenyekiti wa ATE alalamikie uwakilishi mdogo wa waajiri. Kazi yangu nimemaliza, sasa iko kwa wawakilishi wenu kutumia vizuri fursa waliyopata kupigania haki na maslahi ya wafanyakazi bila ya kusahau maslahi ya Watanzania wengine. Bahati nzuri wajumbe wengi ni wafanyakazi hata kama hawakuingia Bungeni wakiwa moja kwa moja wanawakilisha wafanyakazi. Kwa hiyo ni rahisi kwa masuala ya wafanyakazi kutetewa. Hamna budi kuwasiliana nao.
Jambo muhimu kwenu kufanya ni kujipanga vizuri kwa hoja za kuwapa wawakilishi wenu kuzipigania. Msipofanya hivyo mtakuja kujikuta wawakilishi wenu wakatekwa na makundi yenye agenda na misimamo isiyoendeleza maslahi yenu. Sisemi wasijihusishe na mambo mengine yenye maslahi kwa taifa, la hasha!. Ninachosema wasifanye hayo na kuacha kusemea yenye maslahi ya wafanyakazi. Wanaweza kukosekana watu wa kuyasemea mkajutia fursa hii.
Naungana nanyi kusikitika kutokana na mienendo na kauli zisizoridhisha za baadhi ya Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba. Naungana nanyi pia kuwasihi watumie lugha ya staha na wazo la kutafuta majawabu kwa njia ya mashauriano itatuwezesha kumaliza tofauti za kambi. Nawasihi waliotoka Bungeni warejee pale Bunge Maalum la Katiba litakapoanza upya baada ya mapumziko ya kupisha Bunge la Jamhuri na Baraza la Wawakilishi kufanya shughuli za lazima hususan bajeti za Serikali zetu mbili.
Hitimisho
Ndugu Kaimu Rais wa TUCTA, Katibu Mkuu na Wafanyakazi Wenzangu;
Naomba nimalize kwa kurudia kuwashukuru tena kwa kunipa nafasi hii adhimu ya kujumuika nanyi tena katika sherehe za mwaka huu. Napenda kuwahakikishia, kwa mara nyingine tena, kwamba dhamira yangu binafsi, na ile ya Serikali ninayoiongoza ya kutatua changamoto zinazowakabili wafanyakazi iko palepale. Kilio chenu ni kilio changu. Tumejitahidi katika kipindi hiki kutatua matatizo ya wafanyakazi na mafanikio yake mnayaona. Nina imani kuwa tukishirikiana katika mwaka mmoja uliobakia tutaweza kutatua kero nyingi zaidi.
Mwisho, napenda kuwakumbusha kuwa, maslahi mazuri kwa wafanyakazi yana uhusiano wa moja kwa moja na kuongezeka kwa tija, uzalishaji, na pato la waajiri katika sekta binafsi na sekta za umma. Shime nawasihi muongeze juhudi ili nanyi mnufaike zaidi. Kwa upande wangu naamini kwamba neema haiko mbali sana. Tumefanikiwa kuweka misingi mizuri ya kiuchumi, tumeunda taasisi na kuweka mazingira mazuri ya kisheria na kisera. Bahati nzuri Mwenyezi Mungu ametushushia neema ya rasilimali ikiwemo gesi asilia. Vyote hivi kwa pamoja, vinatupa matumaini kuwa ndoto yetu ya kufikia nchi ya uchumi wa kati mwaka 2025 itatimia. Inawezekana Timiza Wajibu Wako.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni sana kwa kunisikiliza. Nawatakia sherehe njema.