Aliyewahi kuhudumu kama Balozi wa Tanzania nchini Nigeria na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Eswatini na Namibia, Timothy Bandora (72), amefariki dunia jijini Nairobi, nchini Kenya, ambako alikuwa akipatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa ratiba ya msiba iliyotolewa na familia, marehemu anatarajiwa kuzikwa Jumanne, Desemba 16, 2025, katika Makaburi ya Kinondoni huku ibada ya mazishi ikifanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Msasani, jijini Dar es Salaam.
Bandora, Mwanadiplomasia nguli wa Tanzania, amewahi kuhudumu katika awamu ya kwanza hadi ya tatu akitekeleza majukumu mbalimbali ya kitaifa na kimataifa katika utumishi wa umma pamoja na ndani ya Umoja wa Mataifa (UN).
Miongoni mwa majukumu aliyofanya wakati wa uhai wake ni kuongoza kurugenzi ya ushirikiano wa kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi wa Tanzania nchini Nigeria ofisi ya Lagos, ambayo pia inahudumia nchi za Benin, Togo, Cote d’Ivoire, Ghana, Guinea, Senegal, Burkina Faso, Mali, Sierra Leone, Liberia, Guinea-Bissau na Mauritania.


