Jeshi la Polisi mkoani Kigoma limethibitisha kuua mtu mmoja ambaye majina yake hayajatambulika, katika tukio la kudhibiti ujambazi ndani ya Ziwa Tanganyika, baada ya majambazi kuvamia wavuvi na kupora zana mbalimbali za uvuvi huku wengine wakielezwa kukimbia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma Filemon Makungu amethibitisha tukio hilo, na kuongeza kuwa watuhumiwa walifuatiliwa na Polisi baada ya raia wema kutoa taarifa.
Katika tukio hilo, majambazi walianza kufyatua risasi kabla ya majibizano kuanza na mtuhumiwa huyo kupigwa risasi na kufariki dunia.
Katika tukio hilo, vitu mbalimbali vimekamatwa ikiwemo silaha, risasi, mashine za wavuvi na nyavu za kuvulia. Kamanda Makungu amewataka wavuvi kufika kituo kikuu cha Polisi Kigoma ili kubaini mali zao.

