Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Ashatu Kijaji
Amesema hatua hiyo ni kutokana na Kanuni za Usimamizi na Udhibiti wa Taka Ngumu za Mwaka 2024 zinazoelekeza wazalishaji wa bidhaa wawajibike na taka wanazozalisha kupitia dhana ya Mazingira na maendeleo endelevu, kuanza kufanyiwa mapitio na Serikali.
Dkt. Kijaji amesema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa zoezi la urejelezaji wa taka ngumu katika Jiji la Dar Es Salaam kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira jijini Dodoma leo Agosti 15, 20204.
Amesema uzalishaji wa taka ngumu unakadiriwa kuwa takribani tani milioni 7 kwa mwaka na kiasi kikubwa kinazalishwa katika Mamlaka za Majiji, Manispaa na Halmashauri za Miji Midogo ikilinganishwa na Halmashauri za Wilaya ambazo nyingi ziko vijijini.
Aidha, urejelezaji wa taka ngumu ni moja ya mbinu ya upunguzaji wa taka katika madampo ambapo inakadiriwa kuwa asilimia 5 hadi 10 ya taka ngumu zinazozalishwa nchini zinarejelezwa zikiwemo za plastiki, karatasi, chuma chakavu, makopo ya aluminiamu na chupa za kioo.
"Shughuli hizi za urejelezaji ni mojawapo ya mikakati ya kuboresha usimamizi wa taka ngumu na kupunguza kiasi cha taka ngumu zinazopelekwa dampo. Hatua hii ni muhimu kwa kuzingatia kuwa taka ngumu zinaweza kuwa malighafi ya kuzalisha bidhaa nyingine pamoja na kutoa fursa za ajira na hivyo kuchangia maendeleo ya kiuchumi, kulinda afya ya jamii pamoja na kuboresha hifadhi ya mazingira,” amesema.
Dkt. Kijaji amesema uwepo wa kiwango kidogo cha taka zinazorejelezwa unatokana na mwitikio mdogo wa utenganishaji wa taka katika ngazi ya kaya na maeneo ya biashara, masoko, viwanda na taasisi katika maeneo mengi ya jiji na Manispaa.