Jumatatu , 27th Oct , 2025

Rais wa Argentina, Javier Milei amekiongoza chama chake katika ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa katikati ya muhula siku ya Jumapili, baada ya miaka miwili ya kwanza ya urais wake wa kubana matumizi na mageuzi ya soko huria.

Chama chake, La Libertad Avanza, kimepata karibu asilimia 41 ya kura, kikichukua viti 13 kati ya 24 vya Seneti na 64 kati ya viti 127 vya mabunge ya chini vilivyokuwa vikiwaniwa.

Mafanikio yake yatarahisisha zaidi kuendelea na mpango wake wa kupunguza matumizi ya serikali na kudhibiti uchumi katika taifa hilo la Amerika Kaskazini,

Kabla ya upigaji kura, mshirika wa Milei, Donald Trump, aliweka wazi kuwa msaada uliotangazwa hivi karibuni na Marekani wa dola bilioni 40 kwa Argentina utategemea ushindi wa Milei.

Wafuasi wa Milei walifurahia hilo, ingawa wakosoaji walimshutumu Donald Trump kwa kuingilia kati uchaguzi wa Argentina.

Milei aliwaambia wafuasi wake waliokuwa wakishangilia: "Lazima tuendelee na mageuzi ambayo tumeyaanzisha ili kuibadilisha historia ya Argentina... ili kuifanya Argentina kuwa kubwa tena."

Kabla ya chaguzi hizi chama chake kilikuwa na viti saba tu vya Seneti na viti 37 katika bunge la chini.

Hiyo ilimaanisha mpango wake wa kubana matumizi na mageuzi ulikumbana na vikwazo mbalimbali vya kisiasa.
Miswada yake ya kuongeza ufadhili kwa vyuo vikuu vya serikali, watu wenye ulemavu na huduma ya afya ya watoto - yote ilibatilishwa na wabunge wa upinzani.