
Akizungumza wakati wa Kusaini Mkataba huo, Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar Dk. Amour Suleiman Mohamed, amesema Mkataba huo ni muendelezo wa makubaliano ya muda mrefu kati ya Bohari ya Dawa Zanzibar (CMS) na Bohari ya Dawa MSD ya kuimarisha upatikanaji wa huduma za dawa zenye ubora zaidi, nchini Tanzania.
Amesema makubaliano hayo yamehusisha masula mazima ya utaalamu wa kuwajengea uwezo watumishi, kuimarisha miundombinu ya Bohari ya Dawa upande wa Zanzibar na Tanzania Bara, uhifadhi wa dawa na vifaa Tiba pamoja na matumizi ya Tehama.
Aidha ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya imeweka vipaumbele vya kuimarisha huduma za afya ikiwemo masula ya dawa kama ilivyoanishwa katika mkataba huo.
Amesema Wizara ya Afya kupitia Bohari ya dawa itaendelea kushirikiana na MSD katika kutoa huduma bora za dawa hasa katika maeneo ya mifumo kwenye uagizajia dawa, Vifaa tiba, uhifadhi na ununuzi wa dawa pamoja na kutafuta fedha kwa ajili ya kuwa na dawa za kutosha.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Mavare Tukai amesema MSD na Wizara ya Afya wana uhusino wa kihistoria ambao umewezesha kuimarisha huduma za dawa kwa kubadilishana uzoefu, wataalamu pamoja na kusadiana kwa karibu pale inapotokea dharura.