Ijumaa , 22nd Sep , 2023

Kiongozi wa junta wa Guinea, Kanali Mamady Doumbouya, amesema mfumo wa demokrasia wa nchi za Magharibi haufanyi kazi barani Afrika, huku akitetea matumizi ya uingiliaji wa kijeshi.

 

Aliuambia mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa mjini New York kwamba bara hilo linateseka kutokana na "mfano wa utawala ambao umewekwa juu ya bara la Avfrika" na ambao "una matatizo ya kuzoea hali halisi ya Afrika".

 "Ni wakati wa kuacha kutufundisha na kuacha kututibu kwa dharau kama watoto," . Kanali Doumbouya alichukua madaraka kwa mapinduzi mwaka 2021, na kumuondoa madarakani rais Alpha Condé.

Alitetea kuchukua hatua hiyo kwa bunge la Umoja wa Mataifa akisema ni "kuiokoa nchi yetu kutokana na machafuko kamili".

Wakati huo, habari za mapinduzi hayo zilipokelewa na umati wa watu waliokuwa na furaha katika mji mkuu, Conakry, kwani wengi walifarijika kwamba Rais Condé alikuwa ameondolewa madarakani.

Lakini nchi hiyo ilisimamishwa kutoka kwa kundi la kikanda, Ecowas, baada ya jeshi kuchukua madaraka, huku viongozi wa kikanda wakitaka kurejea kwa utawala wa kiraia.

Mwaka jana, Kanali Doumbouya alitoa ratiba ya mpito kwa serikali iliyochaguliwa baada ya mazungumzo na Ecowas lakini kumekuwa na maendeleo kidogo katika kuandaa kura, shirika la habari la Reuters linaripoti.

Guinea ni miongoni mwa nchi kadhaa za Afrika Magharibi na Kati ambazo zimeshuhudia mapinduzi katika miaka ya hivi karibuni zikiwemo Mali, Burkina Faso, Niger na Gabon.

Mapinduzi hayo yamelaaniwa vikali na Ecowas, Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa.