Jumamosi , 25th Mar , 2023

Idadi ya watu waliowekwa chini ya uangalizi kutokana na kuchangamana na wagonjwa wa Ugonjwa wa Marburg mkoani Kagera imeongezeka na  kufikia 205 kutoka 193 waliotangazwa na  Mganga Mkuu wa Serikali nchini Prof. Tumain Nagu Machi 23 mwaka huu,  akiwa mkoani humo

.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu   amesema kuwa mpaka sasa hakuna visa vipya vya wagonjwa wala kifo chochote kilichotokea tofauti na vifo vitano vilivyotokea awali na wagonjwa watatu wanaoendelea na matibabu.

"Bado tuna visa nane tu ambavyo vimesababisha vifo vitano, hawa 205 waliowekwa karantini sio wagonjwa, tumewaweka chini ya uangalizi baada ya kubainika kuwa walichangamana na wagonjwa, wanaangaliwa afya zao kwa siku 21, ili kuona kama kuna mtu ataonyesha dalili za ugonjwa huo katika kipindi hicho" amesema Ummy.

Amesema kuwa mgonjwa wa Marburg hawezi kumwambukiza mtu mwingine kama hajaanza kuonyesha dalili zozote, huku akiwataka wananchi kuendelea kujikinga kwa kufuata maelekezo yote wanayoelezwa na wataalamu wa afya, ikiwamo kunawa mikono kila mara, kutumia vitakasa mikono na kuepuka misongamano.

Pia amesema kuwa timu ya wataalamu wabobezi wa kupambana na ugonjwa huo wamekwishawasili mkoani Kagera ili kusaidiana na wataalamu wengine wa afya walioko mkoani humo, lengo likiwa ni kuhakikisha ugonjwa huo unadhibitiwa.