Jumatatu , 28th Dec , 2020

Mchezaji nyota wa klabu ya Juventus ya Italia na timu ya Taifa ya Ureno Cristiano Ronaldo ametwaa tuzo ya Mchezaji bora wa karne ya Dubai Global Soccer ambayo imetolewa na Baraza la Michezo la nchini Dubai usiku wa kuamkia hii leo.

Cristiano Ronaldo

Ronaldo ametwaa tuzo hiyo baada ya kupigiwa kura nyingi na wapenzi na wafuatiliaji wa soka ulimwenguni na kuwapiku Lionel Messi mshambuliaji wa klabu ya Barcelona na timu ya taifa ya Argentina na Robert Lewandoski wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Poland.

Vigezo vilivyotumika kutoa tuzo hiyo kwa Cristiano Ronaldo ni mfumo wa upigaji kura wa wapenzi na wafuatiliaji wa soka nchini kupitia mtandao kwa kuangalia mafanikio ya wachezaji soka kuanzia mwaka 2001 hadi kufikia mwaka huu ambapo kura hizo zikamuangukia CR7.

Ronaldo na Lewandoski

Baada ya kubeba Tuzo hiyo Ronaldo amesema “Sio rahisi kuwa kwenye kiwango cha juu kwenye ushindani huu kwa miaka mingi. Najivunia sana lakini isingewezekana bila ya kusaidiwa na makocha wakubwa na klabu kiujumla”'

“Tuzo ya mchezaji bora wa karne inaongeza thamani kubwa na kutoa uelekeo mzuri sana kwa kila kitu nilichokifanya kwenye miaka yangu 20 katika maisha yangu ya soka”.

Ronaldo amepigiwa kura kuwa mshindi wa tuzo hiyo baada ya kuisaidia klabu yake ya Juventus kuwa mchezaji bora wa Juventus na ligi kuu nchini Italia Serie A kwa kufunga mabao 37 an kutengeneza mabao 7 kwenye michuano yote na kuisaidia Juventus kuwa mabingwa wa Serie A.

Tuzo nyingine zilizotolewa usiku wa hapo jana na Baraza la Michezo nchini Dubai ni pamoja na tuzo ya mchezaji bora wa mwaka 2020 ambayo imeenda kwa mshambuliaji wa Bayern Munich Poland Robert Lewandoski ambaye pia ni mchezaji bora wa mwaka huu kwa tuzo za FIFA.

Robert Lewandoski

Robert Lewandowski amepigiwa kura kuwa mshindi wa Tuzo ya mchezaji bora wa mwaka huu baada ya kufunga mabao 55 na kutengeneza mabao 10 kwenye michezo 47, kuwa mfungaji bora katika kila mashindano aliyeshiriki na kuifanya Bayern kushinda mataji 3 likiwemo la UEFA.

Tuzo ya timu bora ya mwaka imekwenda kwa Bayern Munich ya Ujerumani ambao ndiyo mabingwa watetezi wa tajo la klabu bingwa barani ulaya, ligi kuu nchini Ujerumani, Germany DFB Pokal na Germany Super Cup na kumfanya Kocha wake Hans Flik kuwa kocha bora wa mwaka.

Timu bora ya Karne ni Real Madrid, timu yenye mataji mengi ukanda wa Mashariki na kati ni Al Ahly ya Misri, Jorge Mendes akiibuka na tuzo ya Wakala bora wa wachezaji wa karne na Gerrard Pique na Aliyekuwa mlinda mlango wa Real Madrird Ike Casillas kuwa Career Award.

Kocha bora wa Barcelona tokea klabu hiyo kuanzishwa hadi hivi leo, Pep Guardiola ambaye sasa anainoa klabu ya Manchester City ya Uingereza ametwaa tuzo ya kocha bora wa Karne kuanzia mwaka 2001 hadi hivi leo.

Pep Guardiola

Guadiola amepigiwa kura nyingi ambazo zimemuwezesha kutwaa tuzo hiyo baada ya kuviongoza vilabu vya Barcelona, Bayern Munich na Manchester City kutwaa mataji makubwa ya ligi kuu na la klabu bingwa ulaya mara 2 akiwa na Barcelona na jumla kuwa kocha mwenye mataji zaidi, 29.