Jumatano , 24th Jul , 2019

Katika kuhakikisha wanafunzi wa kike katika shule mbalimbali nchini wanasoma bila kupata changamoto ya kukosa masomo wakati wa hedhi, East Africa Television LTD kupitia kampeni yao ya NAMTHAMINI imeendelea kuwapatia taulo hizo.

Wanafunzi wa kike shule ya msingi Turiani pamoja na walimu wao wakiwa na watangazaji wa East Africa Television na East Africa Radio baada ya kupokea taulo za kike.

Kwa mwaka 2019, shule ya kwanza kupata Taulo hizo ni Shule ya msingi Turiani iliyopo Magomeni Kinondoni Dar es salaam, ambao wao waliomba 'Pieces' 200 kwaajili ya wanafunzi wao.

Timu ya East Africa Television LTD imefika shuleni hapo leo Julai 24, 2019 na kutoa taulo hizo ambapo amekabidhiwa mwalimu mkuu Bi. Eligiver Kimaro mbele ya wanafunzi.

Baada ya kukabidhiwa, Bi. Eligiver ameishukuru East Africa Television LTD kupitia kampeni ya NAMTHAMINI kwa kuwasaidia kuwastili wasichana shuleni hapo.

''Niwashukuru sana kwa msaada huu ambao utasaidia sana watoto wetu hapa, maana kwa uwezo wetu tusingeweza kuwapatia taulo za kutosha''.

Aidha msichana Batuli Mohamed mwanafunzi wa darasa la saba, amesema wamekuwa wakipitia changamoto ya kujisikia wanyonge wanapokuwa kwenye hedhi na wanakosa taulo za kike, ambapo sasa hali itakuwa tofauti baada ya kupokea Taulo za kike kutoka East Africa Televison LTD.

Kampeni hii ya NAMTHAMINI, inaendelea kwa mwaka wa tatu ambapo tayari imeshafikia wanafunzi wa kike zaidi ya 3000 nchini.