Jumanne , 11th Dec , 2018

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imedai katika kipindi cha hivi karibuni taasisi hiyo imefanikiwa kushinda kesi zake mbalimbali tofauti na ilivyokuwa kipindi cha nyuma ambapo kesi nyingi zilikuwa ikipigwa chini.

Mkurugenzi wa TAKUKURU Diwani Othman.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU nchini, Diwani Athuman, katika kipindi cha mwaka mmoja taasisi hiyo imeokoa Sh 70.3 bilioni zilizokuwa ziingie mifukoni mwa wala rushwa.

Diwani Athuman ameyasema hayo leo Jumanne Disemba 11, 2018 Jijini Dodoma katika ufunguzi wa mkutano mkuu wa makamanda wa taasisi hiyo wa mikoa na maofisa wake mbalimbali ambapo amesema mapambano dhidi ya rushwa bado ni vita kubwa inayohitaji ujasiri.

Aidha amesema katika kipindi cha mwaka mmoja kesi 495 zimefunguliwa na nyingi kati ya hizo wameshinda.

Diwani amesema katika uongozi wake wa miezi mitatu ndani ya taasisi hiyo amebadili mfumo wa utendaji na mtazamo, na kwamba anashirikiana na wenzake kuwapeleka watu mahakamani bila kuzingatia ukubwa wala muonekano wa nafasi zao.

Hivi karibuni Taasisi hiyo ilimuita kiongozi Mkuu wa Chama ACT - Wazalendo Zitto Kabwe kwa ajili ya mahojiano juu ya kutoa taarifa za rushwa na uhujumu wa miradi ya makaa ya mawe na chuma ya Mchuchuma na Liganga.