Jumapili , 11th Feb , 2018

Klabu ya soka ya Azam FC leo imesafiri kuelekea mkoani Kagera kwaajili ya mchezo wa ligi kuu dhidi ya Kagera Sugar, ambapo msemaji wa timu hiyo Jaffary Idd amesema tofauti ya alama kati yao na Yanga haiwavunji moyo.

Akiongea kabla ya safari Jaffary Idd amesisitiza kuwa wamejipanga kuhakikisha wanapata ushindi ili kuendelea kuwa kwenye mbio za ubingwa licha ya mechi yao ya raundi ya 17 dhidi ya Simba kupoteza jumatano wiki hii.

''Kimsingi sisi tumejiandaa vizuri, tunakwenda kucheza kwenye uwanja bora wa Kaitaba, kwahiyo aliyejiandaa vizuri atashinda, na tunataka kushinda ukizingatia mbio za ubingwa bado na hata timu ya Yanga iliyopo nafasi ya pili kwa tofauti ya alama moja haituvunji moyo'', amesema.

Mchezo huo wa raundi ya 18 ligi kuu soka Tanzania Bara kati ya Kagera Sugar na Azam FC utachezwa kesho jumatatu na baada ya hapo Azam FC itarejea jijini Dar es salaam kabla ya kusafiri kuelekea Iringa kucheza na Lipuli FC.

Kwa upande wa Kagera Sugar mambo si mazuri wakiwa katika nafasi ya 15 kwa alama 13 baada ya michezo 17 huku wakilingana alama na timu inayoshika nafasi ya mwisho Njombe Mji yenye alama 13 katika mechi 17.