Baadhi ya wanamichezo wa michezo ya UMITASHUMTA wakishangilia katika moja ya michezo yao.
Michuano ya michezo ya shule za msingi UMITASHUMTA mkoa wa Dar es salaam iliyokuwa ikifanyika katika viwanja vya chuo kikuu cha Dar es salaam sehemu ya mlimani ikishirikisha kombani za shule za msingi toka wilaya za Ilala, Kinondoni na Temeke imemalizika hii leo
Afisa michezo toka ofisi ya mkuu wa mkoa Dar es salaam Adolf Halii amesema michezo hiyo imekuwa na mafanikio makubwa hasa kutokana na Halmashauri za wilaya kufanya maandalizi ya kutosha kwa timu zao kitu ambacho kitapelekea mkoa wa Dar es salaam kupata kikosi bora kwa ajili ya michuano ijayo ya UMITASHUMTA taifa.
Naye kocha mkuu wa timu ya mpira wa wavu ya Jeshi Stars Lameck Mashindano ambaye alikuwa katika michuano hiyo akisaka vipaji na pia kulisaidia jopo la walimu katika kuunda kikosi cha mkoa kwaajili ya mashindano ya Umitashumta taifa amesema mashindano hayo yamesheheni vipaji na ana uhakika wa timu hiyo kuendelea kutesa katika michuano ya taifa na hata kutoa vipaji vitakavyochukuliwa na timu mbalimbali kote nchini.