Jumatano , 1st Mar , 2017

Kituo cha East Africa Television LTD (EATV) kimezindua kampeni ya kuchangisha fedha za kwa ajili ya ya kununulia taulo za hedhi (Pedi) kwa ajili ya wanafunzi wa kike katika Shule za Sekondari nchini Tanzania.

Kituo hicho namba moja kwa vijana nchini Tanzania kitaendesha kampeni hiyo inayokwenda kwa jina la ‘NAMTHAMINI’ ikiwa ni sehemu ya aadhimisho ya Siku Wanawake Duniani (Machi 8)

Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam Afisa Masoko wa EATV ambaye ndiye Mratibu wa Kampeni hiyo Brendansia Kileo amesema fedha zote zitakazokusanywa katika kampeni hiyo zitatumika kununulia pedi na kusambazwa kwa wanafunzi wa kike katika shule za sekondari zitakazochaguliwa nchini Tanzania kwa mwaka mmoja na hivyo kumuwezesha mtoto wa kike kuhudhuria shule bila ya kukosa kwa sababu ya hedhi.

“Kumekuwepo na tatizo la wanafunzi wa kike kukosa kuhudhuria shule kwa kati ya siku tano hadi saba kutokana na kukosa pedi za kujisitiri wakati wa hedhi, ambapo kwa mwaka inakadiriwa mwanafunzi wa kike hukosa kuhudhuria shule kwa siku 60 hadi 70 kutokana na kukosa pedi tu, hali ambayo inachangia kutofanya vizuri kimasomo”. Amesema Brendansia.

Brendansia Kileo - Afisa Masoko EATV

Kuhuusu malengo, Brendansia amesema lengo ni kukusanya pedi angalau kwa ajili ya wanafunzi 1500 na kila mwanafunzi apate pedi za angalau mwaka mzima, na kuhusu kuchagua ni shule gani zinufaike, amesema watashirikiana na asasi za kiraia, ili kujua maeneo yenye uhitaji zaidi nchini Tanzania.

Ameongeza kuwa michango yote itakayotolewa itakuwa wazi kwa jamii na pesa zote zitatumika kwa kazi hiyo na hadi tarehe 8 takwimu zote za benki zitachapishwa na kuwekwa hadharani ikiwa ni pamoja na kiasi cha fedha ambacho kimetakuwa kimepatikana

Joyce Kiria - Mkurugenzi HAWA Foundation

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Haki za Wanawake, (HAWA Foundation) ambayo inashirikiana na EATV katika kampeni hiyo, Joyce Kiria, , hawawezi kuwafikia watoto wote Tanzania lakini ujumbe mkubwa ni kuitaka serikali iliangalie suala hilo ili ikiwezekana bidhaa hizo ziondolewe kodi.

Joyce amesema amesema ingawa kilele cha kampeni hiyo ni tarehe 8 Machi mwaka huu, harakati za kuchangisha na kuishawishi serikali iondoe kodi zitaendelea baada ya tarehe hiyo, na kuwataka watu wenye uwezo wa kutoa pedi zenye ubora watoe, na wenye uwezo wa kuchangia fedha wafanye hivyo.

Ili kuchangia kampeni hiyo, kila mwananchi atakayeguswa atapata nafasi ya kuchangia kiasi cha kuanzia shilingi 5,000/ au zaidi kwa kutuma fedha hizo kupitia kwa M-PESA Code Namba 5530307 ama kupitia akaunti ya CRDB Namba 0150258750600.

Kupitia kampeni hiyo EATV LTD pamoja na njia nyingine itatumia vituo vyake vya Radio na TV, ambavyo ni EATV (Channel 5) na East Africa Radio kuhamasisha uchangiaji wa fedha hizo huku taasisi ya HAWA  ikihusika na kupokea, kusimamia fedha zote zitakazochangishwa na kusimamia ununuzi na usambazaji wa pedi hizo mashuleni.

#NAMTHAMINI