Nahodha wa Simba Musa Hassan 'Mgosi' [kushoto] akijaribu kumtoka beki wa Mtibwa Sugar.
Klabu ya soka ya Simba ikicheza mchezo wa pili mfululizo bila nyota wake kadhaa wa kikosi cha kwanza kama Hamis Kiiza, Jurko Murshid, Jonas Mkude, Vicent Agban hii leo ikiwa ugenini imeibuka na ushindi wa kwanza baada ya mechi nne za Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara VPL , kufuatia kuichapa bao 1-0 timu ya Mtibwa Sugar mchezo uliochukua nafasi katika uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro.
Shujaa wa Simba SC katika kipute hicho alikuwa kiungomtukutu mwenye kipaji Abdi Hassan Banda aliyefunga bao hilo pekee kunako dakika ya 70 kwa kichwa maridhawa kwa ufundi mkubwa akimzidi maarifa beki wa pembeni wa timu ya mtibwa Idrisa Rashid 'Baba Ubaya' akimalizia krosi nzuri ya beki wa kushoto, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
Tangu iifunge mabao 2-0 timu ya Wagosi wa Kaya Coastal Union mjini Tanga, Simba haijashinda mechi nyingine ya Ligi Kuu hadi iliposhinda tena hii leo katika dimba la Jamhuri.
Katika michezo iliyopita Simba ilifungwa nyumbani bao 1-0 na Toto Africans ya Mwanza, ikatoa sare ya 0-0 na Azam FC, ikafungwa 1-0 na Mwadui FC zote ikicheza katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kabla ya kutoa sare ya 0-0 na Majimaji mjini Songea katikati ya wiki.
Ushindi huo unaifanya Simba SC ifikishe pointi 62 baada ya kucheza mechi 29 ikiendelea kukamata nafasi ya tatu nyuma ya Azam FC yenye pointi 63 na mabingwa Yanga, wenye pointi 72.
Mchezo mwingine wa ligi hiyo uliopigwa, ni kati ya wageni Azam FC ambao wameibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji African Sports katika uwanja wa Mkwakwani,jijini Tanga matokeo ambayo si mazuri kwa wanakimanumanu hao ambao wanapigana kubaki daraja wakiwa na alama 26 na mchezo mmoja mkononi wa kufunga dimba ugenini huko Manungu Turiani mkoani Morogoro dhidi ya wakata miwa Mtibwa Sugar waliochapwa bao 1-0 na Simba.
Mabao ya Azam FC yamefungwa na mshambuliaji Mkenya Allan Wanga dakika ya 10 na beki Erasto Nyoni dakika ya 74, wakati la Sports limefungwa na Omary Ibrahim dakika ya 11.
Mchezo mwingine ni kati ya wenyeji Mbeya City ambao walibanwa mbavu na Mwadui FC baada ya kutoka sare tasa ya 0-0.