Alhamisi , 5th Mei , 2016

Serikali imekanusha madai ya kutoa maelekezo kwa uongozi wa vyuo vya elimu ya juu ya kuwanyanyasa wanafunzi wa vyuo hivyo wanaojihusisha na masuala ya siasa na badala yake imewataka wafuate kanuni na taratibu zilizowekwa sehemu husika.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Hata hivyo imesema itaendelea kuwahudumia Watanzania wote ikiwemo kutoa elimu kuanzia ngazi awali hadi elimu ya juu bila kujali ya itikadi za dini wala vyama vyao vya siasa.

Waziri Mkuu, Kassm Majaliwa ameyasema hayo leo (Alhamisi, Mei 5, 2016) wakati akijibu swali la papo kwa papo la Mheshimiwa Ester Matiko (Viti maalum Chadema) aliyetaka kujua kama Serikali imetoa maelekezo kwa uongozi wa vyuo vikuu kunyanyasa wanafunzi wanaojihusisha na masuala ya siasa.

“Nakanusha si kweli kwamba kuna maelekezo kwenye vyuo vyote vya elimu ya juu na pia hakuna unyanyasaji wowote wa vyuo na Watanzania wote wanao uhuru wa kujiunga na vyama vyote wanavyovitaka, lakini kila eneo limeweka utaratibu wake hivyo wafuate taratibu na sheria katika sehemu husika,” alisema.

Amesema, sheria za nchi haziruhusu mtu yeyote kufanya siasa vyuoni au pahala pa kazi hususani kwa watumishi wa umma. "Mtu anapoanza kufanya katika shule au vyuo inapunguza concetration ya masomo, ndiyo maana ikaamuliwa hivyo"